Tuesday, July 3, 2012

KUCHAPISHWA KWA MISIMBO YA POSTA (ORODHA ZA POSTIKODI).

Kufuatana na kifungu nambari 41 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inapenda kufahamisha umma kwamba orodha ya Misimbo ya Posta au ‘postikodi’ za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechapishwa kupitia Gazeti ya Serikali Notisi nambari 220 ya tarehe 22 Juni 2012.
Msimbo wa posta (Postikodi) ni mkusanyiko wa tarakimu inayotambulisha eneo la usambazaji wa barua na kwa Tanzania eneo linalotambulishwa ni Kata kwa Tanzania Bara na Wadi kwa Zanzibar.  Kazi hii ya kitaalamu ya kugawa misimbo ya posta imefanyika baada ya utafiti wa muda mrefu ambao umehusisha watalaamu mbalimbali. Ili kuufahamu mfumo wa Msimbo wa Posta wa Tanzania, vigezo vifuatavyo vimetumika kama ilivyofafanuliwa hapa chini.
1. Ufafanuzi wa mfumo wa msimbo wa posta
Mfumo wa msimbo wa posta wa Tanzania utaundwa na tarakimu tano (5) ambazo zinatafisiriwa kama ifuatavyo:
Muundo wa Msimbo wa PostaMaelezo
X X X X XTarakimu 5 (Mfumo wa Tarakimu za Msimbo wa Posta)
X -  -  -  -Tarakimu ya kwanza  = Kanda (1 – 7 tazama (a) hapa chini)
X X -  -  -Tarakimu mbili za kwanza = Mkoa
X X X -  -Tarakimu tatu za kwanza = Wilaya
X X X X XTarakimu zote tano = Kata/Wadi (Eneo la usambazaji)
Tarakimu zote tano = Ofisi ya posta / mteja mkubwa / Eneo maarufu /Misimbo ya posta ya shughuli maalumu.
(a) Tanzania imegawanywa katika kanda 6 na Zanzibar kama ifuatavyo;
1 – Dar es Salaam
2 – Kaskazini
3 – Ziwa
4 – Kati
5 – Nyanda za Juu Kusini
6 – Pwani
7 – Zanzibar
KANDA ZA MISIMBO YA POSTA


(b) Tarakimu ya kwanza na ya pili ya msimbo wa posta (kwa pamoja) inawakilisha mkoa katika Tanzania
(c)  Tarakimu ya kwanza, ya pili na ya tatu (kwa pamoja) inawakilisha Wilaya au Eneo la kati la Biashara katika Wilaya
(d) Tarakimu ya kwanza hadi ya tano ya msimbo wa posta inawakilisha Kata, Wadi, Watumiaji wakubwa wa posta, Vitu maarufu na Shughuli maalumu 
MIFANO YA MISIMBO YA POSTA;
11707: Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
23101: ICC, Arusha
33106: Kirumba, Mwanza
41105: Makole, Dodoma
57103: Mfaranyaki, Songea
63219: Msanga Mkuu, Mtwara
73104: Mkokotoni, Unguja
74209: Wawi, Chake Chake
1. 2.   Vigezo vilivyotumika kugawa misimbo ya posta (postikodi)
KigezoMaelezo
1Eneo la UtawalaKata au Wadi imechaguliwa kuwa eneo la chini la usambazaji.
2Ofisi za PostaKila Ofisi ya Posta itakuwa na msimbo wa posta. Mteja mwenye S.L.B katika Posta fulani atatumia Msimbo wa posta (postikodi) ya Posta ile.
3Watumaji wa barua wakubwaWatumaji wa barua wakubwa kama Wizara za Serikali, Taasisi za Umma, Taasisi za Udhibiti, Makampuni, Taasisi za Kimataifa, Taasisi zisizo za kiserikali zitapewa msimbo maalumu wa posta.
4Vitu maarufuEneo au umbo la kitu ambacho kimehifadhiwa kwa sababu ya kuhifadhi historia litapewa msimbo maalumu wa posta.
5Matukio au shughuli maalumu  (Kwa muda)Kutakuwa na misimbo ya posta ambayo itahifadhiwa kwa ajili ya kugawanywa endapo kutakuwa na shughuli maalumu katika nchi.
  1. 3.   Anuani mpya zitawezesha ufikishwaji majumbani barua na vifurushi. Kwa mfano anwani kamili inatolewa hapa chini:
Amos Mbawala
20 Barabara ya Mashele
23101 ARUSHA
              2 – Kanda – Kasikazini
                              23 -  Mkoa – Arusha
                                231 – Wilaya – Arusha
                                   23101 –Kata – Sekei
Orodha ya ‘Postikodi’ imechapishwa kwa ajili ya maeneo ya usambazaji ikijumuisha Mikoa, Wilaya na Kata kama ilivyoainishwa 1 na 2 hapo juu. Orodha ya misimbo ya posta (postikodi) itatolewa kwa ajili ya vigezo vingine vilivyooneshwa 3-5 hapo juu.
Umoja wa Posta Duniani ambacho ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye wajibu wa kuendeleza sekta ya posta katika nchi wanachama, utaarifiwa rasmi ambapo utawafahamisha wadau wakuu wote duniani kuhusiana na matumizi ya mfumo mpya katika Tanzania.
Imetolewa:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.


LEO NI MIAKA 20 TANGU KUTUNGWA KWA SHERIA YA KURUHUSU VYAMA VINGI; BADO UPINZANI NI SAWA NA UADUI!

Ndugu zangu, 
Tarehe kama ya leo miaka 20 iliyopita, yaani tarehe 2 Julai, 1992, Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya kuruhusu kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi. 
Miaka 20 imetimu, tumepiga hatua, lakini, mpaka hii leo, bado upinzani kwa wengine unatafsiriwa kama ni uadui, na wakati mwingine ni uhaini. 
Na katika Tanzania yetu, wenye fikra za kukipinga Chama tawala, CCM na Serikali wamekuwa wakitengwa na hata kupewa majina mabaya. Nimeshawahi kumsikia mtu akiambiwa;
“Alaa, unaongea na Lipinzani hilo!” Kana kwamba aliyeitwa ‘ Lipinzani’ hakuwa Mtanzania na binadamu kama wengine.
Na hakika, katika kujadili hili la Katiba Mpya, tuna kila sababu ya kuipitia historia yetu. Maana, naamini, kuwa historia ni mwalimu mzuri. 
Itakumbukwa, katikati ya vuguvugu lile la mageuzi ya kisiasa miaka ya 90 mwanzoni, Watanzania zikatufikia habari; kuwa Oscar Kambona, aliyekosana na Nyerere na aliyekimbila uhamishoni Uingereza, alikuwa njiani kurudi nyumbani. Ujio wa Oscar Kambona ukawa gumzo la mjini na nje ya jiji. Kuna waliojiandaa kwenda uwanjani kumpokea.
Usiku mmoja ikasikika sauti ya Bw. Mrema redioni. Sauti ya Waziri wa Mambo ya Ndani. Mrema alitamka, kuwa kama Kambona angekanyaga mguu wake Dar es Salaam, basi, angekamatwa kujibu mashtaka ya uhaini.
Ni hofu ile ile ya Serikali hata wakati huo. Hofu ya kuimarika kwa fikra za upinzani na kukua kwa upinzani. Mrema akatumika au akajituma kuwatisha na kuwakatisha tamaa Watanzania. Kambona alikanyaga Dar, hakuwa na mashtaka ya kujibu. Ulikuwa ’ mkwara’ tu, kama wanavyosema mitaani.
Na Mrema, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliifanya kweli kazi ya kuwa ’ Mbwa wa Serikali’. Alibwaka kweli kweli. Nakumbuka usiku mmoja mwanzoni mwa miaka ya tisini nilimsikia Mrema akiongea redioni kutishia maandamano ya CUF. Maandamano yale yalikuwa yahitimishwe kwa mkutano viwanja vya Mnazi Mmoja. Mwenyekiti wa CUF, Bw. James Mapalala ndiye alikuwa aongoze maandamano hayo na kuhutubia.
Augustino Lyatonga Mrema akaaunguruma redioni usiku ule. Alishusha ’ mkwara’ mzito. Kuwa maandamano hayo si halali na yangekutana na nguvu za dola. Kesho yake, CUF waliingia mitaani. Ndio, Ungangari wa CUF ulianza siku nyingi.
Pale Mnazi mmoja FFU wakamwagwa, na farasi wao pia. Virungu vilitembea. James Mapalala, Mwenyekiti wa CUF, hakuonekana. Kukawa na taarifa, kuwa anatafutwa na polisi.
Dar ilikuwa ndogo wakati huo, lakini James Mapalala hakupatikana .
Ninazo taarifa za kuaminika za Kibalozi, kuwa James Mapalala alikuwa amejificha kwenye moja ya makazi ya rafiki yake, balozi wa nchi moja ya Kimagharibi. Ni balozi gani huyo? Na nini hasa kilitokea miaka 20 iliyopita?
James Mapalala yungali hai. Huu ni wakati kwa waandishi vijana kuwatafuta wazee veterani wa harakati za mageuzi ya kisiasa hapa nchini. Wazee kama akina James Mapalala.
Hawa ni watu muhimu sana watakaotusaidia kupokea simulizi zao. Kisha ziwekwe kwenye maandishi, na iwe kumbukumbu za kihistoria. Ni historia yetu, tusiionee aibu. Ni urithi tutakaowaachia wajukuu zetu ili nao waweze kujifunza. Waweze kujitambua na kujenga mioyo ya uzalendo.
Na.Blogger Maggid Mjengwa.