Saturday, January 21, 2012

Mhadhara wa Lagos ameahirishwa



Wakaazi wa mji wa KANO, kaskazini mwa Nigeria, wanasema wamehisabu maiti zaidi ya 20, baada ya mashambulio ya mabomu hapo Ijumaa usiku.
Kikundi cha wapiganaji wa Kiislamu, Boko Haram, kinadai kuwa kilifanya mashambulio hayo dhidi ya makao ya polisi pamoja na vituo vengine vya polisi na maofisi ya serikali.
Amri ya kutotoka nje imewekwa katika mji wa Kano.
Na waratibu wa mhadhara uliopangwa kufanywa leo mjini Lagos, kuipinga serikali, wamevunja mkutano huo kwa sababu ya mashambulio ya jana.
Kundi la watetea haki za raia, liitwalo Save Nigeria, limevunja mhadhara mkubwa uliopangwa kufanywa leo, ambapo watu maelfu wakitarajiwa kutaka wakuu wawaondoe wanajeshi katika mji mkuu wa biashara, Lagos, na wapambane na rushwa nyingi ndani ya serikali.
Waratibu wanasema mashambulio ya kigaidi ya jana dhidi ya vituo vya polisi katika mji wa pili kwa ukubwa, Kano; pamoja na wasiwasi kuwa magaidi wanaweza kushambulia mhadhara piya na kuuwa watu, imewapelekea kuwaambia wafuasi wao wabaki majumbani mwao.
Polisi wameshawahi kutumia moshi wa kutoza machozi dhidi ya waandamanaji mapema juma hili, na serikali ilituma wanajeshi kukalia uwanja ambapo mhadhara ungelifanywa.

Chanzo.BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment