Thursday, January 19, 2012

Rais Jakaya Kikwete Atuma Salaam Za Rambimrambi Kufwatia Kifo Cha cha Mhe. Jeremia Solomon Sumari,Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa Tiketi ya CCM na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho  Kikwete
--- 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho  Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.,) kutokana  na kifo cha Mhe. Jeremia Solomon Sumari, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la 
Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM na Naibu Waziri wa Fedha na  Uchumi, kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 19 Januari, 2012  katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa 
matibabu.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa  za kifo cha Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari kwani alikuwa kiongozi  aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake la Uchaguzi la Arumeru  Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhfa wake wa Waziri kwa umahiri  na uhodari mkubwa”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais  Kikwete amesema kutokana na kifo chake, wananchi wa Arumeru Mashariki 
wamepoteza kiongozi wa kutegemewa sana huku Taifa likiachwa na pengo  kubwa ambalo si rahisi kuzibika ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi  katika Wizara ambayo ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
“Kwa dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi  kwa familia ya Marehemu Jeremia Sumari kwa kumpoteza kiongozi na  mhimili madhubuti wa familia. Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja 
nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na namuomba Mwenyezi Mungu,  mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya Marehemu Jeremia Solomon Sumari  mahali pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Ameiomba  familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi  hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni  mapenzi yake mola.

Imetolewa na
Kurugenzi Ya Mawasiliano 

IKULU 
19 Jan 2012

No comments:

Post a Comment