Afisa wa benki ya CRDB tawi la Singida,Emmanuel Kafui (wa kwanza kushoto) mratibu wa tamasha la michezo linalotarajiwa kufanyika jumamosi hii mjini Singida,akizungumza na mwandishi wa MO BLOG. Kulia ni msaidizi wake, Mbwana Ahmed.(Picha na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu
Benki ya CRDB tawi la Singida mjini kupitia akaunti yake ya Scholar kwa kushirikiana na wadau wengine, imeandaa tamasha kabambe la michezo mbali mbali litakalohudhuriwa na vyuo vinne vilivyopo mjini Singida.
Tamasha hilo la aina yake na ambalo ni la kwanza kufanyika mkoani Singida, linatarajiwa kufanyika jumamosi April 28 mwaka huu, kuanzia saa tatu asubuhi, hadi saa kumi jioni.
Vyuo vitakavyoshiriki tamasha hilo ni chuo cha uhasibu (TIA) tawi la Singida, uhazili (TPSC), VETA na chuo cha walimu.
Akizungumza na Mwandishi wa MO BLOG, mratibu wa tamasha hilo, afisa wa CRDB benki Singida, Emmanuel Kafui, alitaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni mpira wa miguu, mpira wa pete, uwezo wa kunywa soda, kukimbiza kuku, kuvuta kamba na riadha.
Kafui alisema lengo la tamasha hilo ,ni kuhamasisha wanafunzi wa vyuo kujua wajibu wao kwa jamii, ushiriki wa vijana katika elimu ya uzazi, kutangaza biashara na umuhimu wa kushirika michezo kwa ajili ya kuboresha afya zao.
Alisema mgeni rasmi katika tamasha hilo la michezo, anatarajiwa kuwa katibu tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan.
Kafui alitaja wadhamini wengine wa tamasha hilo kuwa ni shirika lisilo la kiserikali la HAPA kupitia kitengo cha YMC na kampuni ya vinywaji baridi ya Bonitte Bottlers kupitia kinywaji chake cha Coca cola.
“Naomba nitumie nafasi hii kuwaalika wakazi wote wa hapa mjini na vitongoji vyake, wahudhurie tamasha hili kabambe, ili kupata burudani ya aina yake na pia wapate ujumbe mbali mbali ikiwemo juu ya huduma zitolewazo na CRDB”,alisema Kafui.
No comments:
Post a Comment