Monday, April 30, 2012

ONYESHO LA ZIARA ZA WASHINDI WA TUZO ZA KILIMANJARO PREMIUM LAGER MJINI DODOMA.






Wasanii chipukizi tatu bora wa liovumbuliwa na ziara ya washindi wa tuzo ya muziki ya Kili 2012 mjini Dodoma.
Mashabiki wa muziki wa kizazi kipya Mjini Dodoma, Mwishoni mwa wiki walipata fursa ya kuwashuhudia vinara wa tuzo za muziki za Kilimanjaro, katika tamasha babu kubwa lililofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Mkali wa mapigo ya muziki wa R&B Ben Pol alifanya kazi ya ziada kuzuia shati lake lisivuliwe na msichana, aliyeitwa na msanii huyo jukwaani ili kucheza naye.
Tukio hilo lilimkuta nyota huyo Ben Pol ambaye mwaka huu amenyakua tuzo ya wimbo bora wa R&B, akiwa kama mwenyeji wa Mkoa wa Dodoma alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kuimba wimbo uliompa tuzo wa Number One Fun.
Diamond alitoa burudani ya aina yake akithibitisha kwa wakazi wa Dodoma kwamba alistahili tuzo tatu alizozipata.
Aliendelea na kuimba nyimbo zake mbalimbali na kufanya mashabiki kumshangilia muda wote.
Msanii aliyejinyakulia tuzo ya Zuku rumba Ali Kiba alifunika kwa kucheza pamoja na wacheza shoo wake ambao walionyesha umahiri wa hali ya juu.
Nae  Ommy Dimpoz, alitambulisha wimbo wake mpya katika onyesho la vinara wa tuzo za muziki za Kilimanjaro .
Msanii huyo ambaye mwaka huu alifanikiwa kuchukua tuzo mbili, ikiwa ni ile ya msanii chipukizi na tuzo ya wimbo wa kushirikiana.Wimbo uliyompatia tuzo hizo mbili ni ule wa Nai Nai.
Dimpoz alipanda jukwaani na madansa wake na kuanza kuimba wimbo huo mpya uitwao Baadae.
Msanii aliyenyakua tuzo ya wimbo bora wenye vionjo vya asili AT, alirusha shati lake kwa mashabiki, ambao walilidaka na kuanza kuligombania.
Fujo hizo ziliendelea kwa takribani dakika 30 kila mmoja akilivuta shati hilo, mithili ya watu wanaolikamua maji, lakini baadaye mmoja wao alifanikiwa kulipata.
Rapa aliyechukua tuzo mbili R.o.m.a Mkatoliki, alikuwa ndio wa mwisho kupanda stejini, ambapo alitanguliwa na Dj Choka, ambaye alianza kufanya mbwembwe kabla ya msanii huyo kupanda na kuacha uwanja mzima kulipuka kwa makelele.
Rapa huyo alipanda na kuanza kukamua kisawasawa, kisha kumalizia kibao kilichompa moja ya tuzo zake Mathematic.
NYOTA kutoka Tanzania House Of Talent (THT), Barnaba amejitolea kumdhamini chipukizi wa muziki wa kizazi kipya wa Dodoma, Juma Madaraka.
Barnaba amejitolea kumsaidia chipukizi huyo ili kuweza kurekodi nyimbo zake kwa fedha zake mwenyewe.
Katika onyesho hilo mashabiki wengi walifurika katika uwanja huo, ambapo msanii chipukizi wa mkoa huo Issa Dubart alikuwa mshindi katika shindano la kusaka vipaji vya tuzo ya Muziki ya Kilimanjaro na kuwashinda Juma Madaraka na Halima Ramadhani.


No comments:

Post a Comment