Thursday, April 26, 2012

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI ATAKA WAWEKEZAJI KUJIKITA KWENYE VITO

Ashura Mohamed-Arusha

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja amewataka wawekezaji wa madini kuhakikisha wanajikita zaidi kwenye  ukataji na ung’arishaji wa vito ili kuongeza thamani ya madini hapa nchini.

Angeleja ameyasema hayo  wakati akifungua maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya madini na vito jijini Arusha yaliyowajumuisha wadau mbalimbali wa madini wakiwemo wanunuzi wakubwa na wauzaji kutoka ndani na nje ya nchi

Aidha aliwataka wawekezaji kwenye sekta ya madini kuwekeza kwenye ukataji na ung’arishaji wa madini ili kuongeza ajira nchini na ukusanyaji kodi hatua itakayoongeza pato la taifa.

Ngeleja ameongeza kuwa  serikali ilizuia usafirishaji nje  wa madini ya tanzanite yasiyoongezewa thamani ya ukubwa wa gramu moja na kuendelea ili kuwajengea uwezo watanzania waweze kukata na kung’arisha madini hapa hapa nchini.

Amesema kwa miaka mingi idadi kubwa ya madini yazalishwayo nchini yamekuwa yakisafirishwa yakiwa ghafi, na kuisababisha nchi kukosa mapato.

Waziri Ngeleja alisema mwaka jana serikali ilianzisha utaratibu wa kuhakikisha madini ya Tanzanite yanaonyesha kuwa yanatoka Tanzania yaani ‘certificate of origin’ kabla ya kuyasafirisha kuyapeleka nje ya nchi.
 Amefafanua kuwa serikali inachokitaka ni kufanya  ni kuhakikisha kuwa  Tanzania inakuwa ndio kituo cha ununuzi wa madini badala ya kwenda kununua nje ya nchi ,ndio lengo haswa tunalotarajia kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeweza kuwapatia watu wengi ajira na kuondokana na umaskini’alisema Ngeleja.

Aliongeza kuwa  hatua hii itasaidia sana kuongeza ajira kwa watu  na serikali kupata mapato ya kutosha kutoka kwenye sekta ya madini.

Aliwahakikishia wawekezaji kuwa serikali itatoa leseni kwa wale watakaojiingiza kwenye eneo hilo na kutambuliwa kama wawekezaji.

Waziri huyo alisema serikali itaendelea kusisitiza uwekezaji kwenye uzalishaji wa vito hapa nchini kabla ya kusafirisha nje.

Alisema hatua hii itawekezekana kutokana na ushirikiano uliopo baina ya serikali na sekta binafsi ndani na nje ya nchi.

“Tunajitahidi kuwaalika wawekezaji kutokana na mazingira mazuri yaliyopo,” alisema na kuongeza kuwa Tanzania ina madini ya aina nyingi ambayo yanatakiwa kuchimbwa.

Maonyesho hayo yameandaliwa na Chama cha wachimba madini nchini (Tamida), na kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchini na nje ya nchi.


No comments:

Post a Comment