Thursday, June 14, 2012

BAJETI YA ZANZIBAR YADAI ONGEZEKO LA KODI KATIKA PETROL, DISELI ADA YA BANDARI NA HOTELI ZA KITALII.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Mh. Omar Yussuf Mzee.
Na.Juma Mohammed, MAELEZO  Zanzibar
Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesomwa jana ikipendekeza  maeneo manane ya kuongeza kodi ikiwemo mafuta ya petrol na dezeli,ada ya bandari, ushuru wa stempu,leseni ya njia, VAT kwa hoteli,mighahawa na watembeza watalii na maeneo mengine.
 Katika hotuba yake ya bajeti kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema  ada ya bandari imependekezwa kuongezwa kutoka shilingi 1,000 ya sasa hadi shilingi 2,000 kwa abiria wanaosafiri baina ya Zanzibar na Tanzania bara.
 Waziri huyo alisema pia kwa upande wa Pemba, Serikali inapendekeza ongezeko la ada kufikia shilingi 1,000 kwa abiria wanaosafiri baina ya Visiwa vya  Unguja na Pemba. Waziri Mzee alisema sheria ya ushuru wa stempu namba 6 ya mwaka 1996 sheria ya kodi za hoteli namba 1 ya mwaka 1995, sheria ya ada za bandari namba 2 ya mwaka 1999, sheria ya ushuru wa petrol namba 7 ya mwaka 2001.
 Waziri huyo alisema Sheria nyengine ni pamoja na ile ya usimamizi na utaratibu wa kodi namba 7 ya mwaka 2009, sheria ya kodi ya ongezeko la thamani namba 4 ya mwaka 1998, sheria ya bodi ya mapato Zanzibar namba7 ya mwaka 1996 na sheria ya mafunzo ya amali namba 8 ya mwaka 2006.
 Aidha, SMZ inapendekeza pia kuongeza ushuru wa ongezeko wa mafuta kwa shilingi 50 kwa lita inayoingia nchini kwa mafuta ya petrol na diseli tu ambapo hatua hiyo inatarajiwa kuiingizia SMZ shilingi bilioni 3.3.Akizungumzia ongezeko la ushuru wa stempu, waziri huyo alisema serikali inapendekeza kuongeza kutoka asilimia moja na nusu ya sasahadi asilimia tatu ambapo wanatarajia kuongeza mapato kwa serikali ya shilingi bilioni 2.10.
 Eneo lingine ambalo linafanyiwa marekebisho ni sheria ya usafiri barabarani inapendekeza kurekebisha kiwango cha leseni za njia ili kiendane na uzito gari au ukubwa wa injini yake.Alisema kiwango cha sasa cha ada ya leseni ya njia shilingi 24,000 kwa gari kwa mwaka hakizingatii matumizi ya njia tofauti za gari.
Waziri huyo alisema kwamba serikali inapendekeza kutozwa shilingi 15,000 kwa kila gari kwa mwaka na shilingi 3,000 kwa chombo cha moto cha magurudumu mawili au matatu hiyo ni kutokana na idadi ya magari nchini inaongezeka kila mwaka na hivyo kuathiri mazingira kutokana na moshi unaotokana na magari hayo.
Aidha katika marekebisho mengine ni yale ya viwango vya ada za huduma mbali mbali zinazotolewa na serikali na taasisi zake baada ya kubainika ada hizo zimepitwa na wakati.
Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha, serikali inakusudia kufanya marekebisho kiwango cha kodi huduma za mahoteli, mikahawa, na kutembeza wageni.
Alisema inapendekeza kuongeza kiwango cha kodi kwa mahoteli, mikahawa na watembeza wageni wasiosajiliwa kwenye VAT kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 18.
Mzee alisema uchumi wa Zanzibar unatarajiw akukuwa kwa asilimia 7.5 kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2011. Waziri alisema mfumko wa bei unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 8.7 kwa mwaka wa 2012 ambapo mwaka jana mfumko wa bei ulikuwa asilimia14.7.
 Alisema kwamba uchumi wa Zanzibar kwa mwaka huu unatarajiwa kuimarika zaidi kutokana na mipango mbali mbali ya serikali katika ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbali mbali.Katika bajeti hiyo SMZ imeweka maeneo ya vipaumbele kama afya, kuimarisha ajira kwa vijana, kuimarisha ustawi wa wazee, kuimarisha elimu, kuimarisha uchumi, pamoja na kuhifadhi mazingira na kukabiliana na tabia nchi.
SMZ katika bajeti yake mwaka huu imepanga kutumia shilingi bilioni mia tatu na saba na mia saba tisini na saba milioni (307, 797m) kwa kazi za kawaida na shilingi bilioni mia tatu na arubaini na moja na mia moja na arubaini na saba milioni (341,147 m).
 Aidha serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni mia sita na arubaini na nane na mia tisa na arubaini na nne milioni (648,944m).


No comments:

Post a Comment