Sunday, June 24, 2012

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi Ahimiza Vijana ndani ya CCM na Jumuiya Zake Kuendelea Kutunza Amani iliyopo na Kujiepusha na Shari inayoweza Kuzaa Balaa


  Mjumbe wa kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha Suleiman Iddi akisisitiza jambo wakati akiufungua Mkutano wa Umoja wa Wapanda Mapiki Piki wa Wilaya hiyo hapo Ukumbi wa CCM Jimbo la Kitope uliopo Kinduni.
Wajumbe wa Umoja wa Wapanda Mapiki Piki wa Wilaya ya Kaskazini “B” wakifuatilia kwa makini hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wao iliyotolewa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ambaye pia ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi hayupo pichani. Ufunguzi huo umefanyika katika Ofisi ya CCM ya Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B. 
---
 Vijana ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake wamesisitizwa kuendelea kutunza amani iliyopo na kujiepuka na shari inayoweza kuzaa balaa na hatimae kuzagaa kwa maafa Nchini. 

Sisitizo hilo limetolewa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya ya Kaskazini B ambaye pia ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wapanda Mapiki Pili wa Wilaya hiyo hapo Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope uliopo Kinduni. 
Mama Asha amesema Vijana hao wanapaswa kuwa waangalifu zaidi kutokana na vitendo vinavyoashiria fujo ambavyo huonekana kukumba zaidi kundi kubwa la Vijana.

 Amesema suala la utunzaji wa Amani linamuhusu kila Mwana Jamii kwani hata Dini zote pamoja na Madhehebu mbali mbali zimekuwa zikihubiri na kuhimiza suala la utunzwaji wa Amani. 

Akizungumzia suala la Uchaguzi Mama Asha aliwahimiza Wajumbe wa Mkutano huo kuhakikisha Wanawachaguwa Viongozi Makini watakaokuwa Mahiri kwenye uendelezaji wa Ushindi wa Chama chao Katika Uchaguzi ujao. 

Alisema Tabia ya Baadhi ya Watu kuchagua Viongozi kwa misingi ya Ukabila na kujuana imepelekea kukitia doa kubwa Chama Hicho ambacho ndio kimbilio la Wanyonge Nchini. “ Ukweli tabia hii mbaya sana inakera na inafaa kuepukwa mara moja kwa vile inapunguza kwa kiasi kikubwa nguvu ya Chama ”. Alisisitiza Mama Asha. 

Mama Asha aliwakumbusha Vijana hao kuendelea kuyatetea Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambayo yalileta faraja kwa Wananchi walio wengi hapa Zanzibar. Alisema Vijana wanapaswa kuwa makini katika kutetea Viongozi wao kutokana na tabia ya baadhi ya watu kuendeleza tabia ya kuhubiri Matusi hadharani hana sababu dhidi ya Viongozi hao. 

Katika kuunga Mkono juhudi za kuendeleza Umoja huo wa Wapanda Mapiki Piki wa Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha amechangia jumla ya Shilingi Laki Tatu Taslimu { 300,000/- } kusaidia kutunisha Mfuko wa Umoja huo. 

Katika Risala yao iliyosomwa na Katibu Msaidizi wa Umoja huo Nd. Ame Pandu Kombo Vijana hao wameahidi kuendelea kuhamasisha Wananchi pamoja na Wanachama katika kuunga mkono Sera za Chama Tawala ambacho ndio kimbilio la Wananchi walio wengi Nchini. Nd. Ame alisema Umoja wao licha ya kazi kubwa wanayoendelea kuitekeleza lakini bado wanakabiliwa na Changa moto mbali mbali zinazokwamisha kutekeleza majukumu yao. 

Alizitaja Changa moto hizo kuwa ni pamoja na ufinyu wa sare wakati wanapokuwa katika shughuli zao za uhamasishajipamoja na Mtaji mdogo wa Umoja wao unaopelekea kushindwa pia kufungua Akaunti Benki. 

Mapema akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wapanda Mapiki Piki Wilaya ya Kaskazini B Nd. Mosi Ame Mosi aliwatahadharisha Vijana hao kuwa mbali na Makundi ya sasa yanayopandikizwa cheche za kuchafua amani ya Nchi katika maeneo mbali mbali hapa Nchini. 
  Na 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu Wa Pili Wa Rais Zanzibar


No comments:

Post a Comment