Wednesday, June 6, 2012

TANZANIA PROFESSIONALS NETWORK (TPN) YAJADILI HALI YA MAENDELEO YA UCHUMI WA NCHI.

Pichani ni baadhi ya wajumbe walioshiriki kongamano la kujadili hali ya maendeleo ya uchumi wa nchi lililoandaliwa na Tanzania Professionals Network (TPN) wakitoa maoni yao huku wengine wakisikiliza kwa makini.

Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya uongozi wa TPN kuwashukuru wote kwa kuweza kufika leo katika kongamano hili, nafahamu baadhi mmeihirisha shuguli zenu nyingine muhimu, na wengine mmetoka nje ya Dar Es Salaam na wengine nje ya nchi kuja kushiriki nasi leo hii.
Nimatumaini yangu kuwa mtashiriki vya kutosha ili tuweze kuja na majibu ya maswali mengi tuliyonayo juu ya hali na maendeleo ya uchumi wa nchi yetu.
Napenda kuipongeza serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa ambazo imefanya katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa watanzania walio wengi.
Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia sita (6%), ikiwa ni moja ya nchi zinazokuwa kwa kasi barani Afrika.
Tumeona maboresho mbali mbali katika nyanja tofauti za uchumi zikiwemo:
1.Sheria mpya  ya madini ya mwaka 2010,
2. kuanzishwa kwa mamlaka ya maeneo maalum ya kiuchumi (Special economic zones),
3.Marekebisho ya mwaka 2012 ya sheria ya makampuni (Companies Act),
4. Utaratibu wa pamoja wa uingizaji wa mafuta nchini (bulk procurement),
5.Uanzishwaji wa ukanda maalum wa kilimo (SACGOT),
6.Sheria ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi (Public Private Partnership) na marekebisho mengine katika maeneo mbali mbali.
Mabadiliko haya yamekuwa chachu katika kuweka nchi yetu katika ramani ya dunia katika kushawishi uwekezaji toka nje (Foreign Direct Investment-FDI), mikataba mbali mbali ya kimataifa, ukuaji wa biashara za ndani, n.k
Lakini pamoja na hatua hii kubwa ya kiuchumi iliyofanywa na serikali yetu ikishirikiana na wadau mbali mbali, nchi yetu bado ina vikwazo vingi sana vinavyohitaji suluhisho la kudumu, na suluhisho la changamoto hizi inahitaji ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, wanataaluma, vyombo vya habari, wanasiasa, jumuiya za kimataifa, n.k.
Baadhi ya changamoto ambazo zinaikabili nchi yetu ni pamoja na mfumuko wa bei ambao sasa umefikia 18.5% ikiwa na zaidi ya mpango wa serikali wa kuwa na mfumuko wa bei wa 6% tu.
Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya hali ya ufanyaji biashara “cost of doing business” na tumekuwa tukifanya vibaya katika ripoti ya benki ya dunia inayofanywa kila mwaka.
Suala la miundombinu ni kubwa na chachu muhimu ya maendeleo ya nchi yoyote, Tanzania bado inakabiliwa na hali ya kutokuwa na umeme wa uhakika, hali mbaya ya usafiri wa reli, barabara, licha ya bandari zetu kufanya vizuri lakini bado uwezo bandari zetu kumudu shehena inayopita hapa ni mdogo, na hali duni ya viwanja vingi vya ndege.
Tanzania bado inakabiliwa na ubora wa chini wa elimu ya  vijana wetu wanaomaliza vyuo vyetu mbali mbali, hili ni suala muhimu sana kwani uchumi wa nchi hauwezi kukua kama ubora wa elimu bado ni duni.
Tunatambua jiihada zilizofanyika katika kujenga shule nyingi na vyuo vingi nchi nzima lakini bado kuna haja ya kuboresha shule hizi ili ziweze kutoa wanafunzi watakaoweza kumudu changamoto za dunia ya sasa.
Kama ilivyo katika sekta mbali mbali, Tanzania sasa imegundulika kuwa na hifadhi kubwa ya gesi, na tunaamini na mafuta pia, kama hatutakuwa na sheria bora za kutuwezesha kunufaika na rasilimali hii, bado itakuwa ni ndoto kama ambavyo imekuwa katika sekta nyingine.
Suala la jumuiya ya afrika mashariki nalo linapaswa kuangaliwa na kujadiliwa kwa kina kwa jinsi gani Tanzania itafaidika kama nchi na kwa mtanzania mmoja mmoja. Kimsingi suala hili hatuwezi kulikwepa isipokuwa tunahitaji maandalizi ya kutosha na tusiwe na haraka ya kuingia katika shirikisho la kisiasa.
Suala la ajira hasa kwa vijana ni moja ya mambo nyeti yanayokaibili nchi yetu leo, na bila ya kuwa na ufumbuzi wa haraka na kudumu katika eneo hili, hii inaweza kuwa chanzo ya vurugu kama tumeweza kuona yaliyotokea katika nchi mbalimbali za kaskazini mwa Afrika na mashariki ya kati “The Arab spring”
Sisi kama wanataaluma wa nchi hii tuna deni kubwa sana la kutoa mchango ambao utasaidia nchi yetu kutatua changamoto hizi na kutoa njia mbadala katika kushirikiana na serikali na sekta binafsi katika jitihada mbali mbali za kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Wazalendo wenzangu ili tuweze kutumiza baadhi ya mambo yaliyotajwa hapo juu kuna haja ya kufanya jitihada za makusudi ili tubadilike namna tunavyofanya mambo yetu “change the way of doing things” ili uweze kupata Tanzania iliyo bora na endelevu.
Madhui ya kongamano letu ni kujenga mustakabali endelevu wa Tanzania ‘’Building the Sustainable future of Tanzania “
Hivyo basi tuna wajibu wa kutimiza dhana nzima ya uongozi bora na si utawala bora pekee yake, tuwe na mazoea ya kufuata sheria, kanuni na taratibu mbali mbali zilizopo, tuimarishe taasisi zote na kuwe na ukweli na uwazi “openness and transparency” katika mambo yote muhimu ikiwa ni pamoja na mikataba mbali mbali ambayo wakuu wa taasisi za umma na serikali wanaingia na pia kuwe na utaratibu wa uwajibikaji “accountability and responsibility”.
Matumizi mazuri ya rasilimali zetu ni muhimu, wote tunajua kwamba nchi yetu la eneo kubwa la bahari kuliko nchi zote ukanda huu, wote tunajua kuwa nchi yetu ina eneo kubwa la ardhi kuliko jumla ya ardhi ya nchi zote nne zilizobaki katika Afrika Mashariki, wote tufahamu kuwa nchi yetu ina mbuga kubwa za wanyama, wote tunafahamu kuwa nchi yetu ina madini mengi kuliko nchi zote za ukanda huu, tuna visiwa vizuri na mambo mengine mengi licha ya kubarikikiwa viu vyote hivyo bado Taifa letu lina amani, umoja na mshikamano kuliko nchi nyingine zote za ukanda huu.
Yote haya ni mazingira mazuri yanayotakiwa yatumike kama mtaji wa aina yake ili utusaidie kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu kulinganisha na wenzetu ili hatimaye basi ifikapo mwaka 2025 basi uchumi ni wa kipato cha kati.
Wazalendo wenzangu, wote mnajua kuwa mwaka 1961 wakati nchi yetu inapata uhuru , uchumi wetu ulikuwa ni sawa au juu ya nchi nyingi zikiwemo nchi za mashariki ya mbali mfano  Korea ya kusini, Singapore, Malaysia n.k swali la kujiuliza imekuwaje wenzetu hawa ndani ya miaka 20 hadi 30 tu walipiga hatua kubwa za kimaendeleo na kutoka katika nchi maskini na kuwa nchi zenye uchumi mkubwa sana duniani ? Kama wao waliweza sisi tushindwe tumekosa nini ?
Ni dhahiri jibu la swali hili ni rahisi tu kunahitajika maono, ujasiri na uthubutu wa kuchukua maamuzi magumu yenye manufaa kwa wengi na si kwa wachache. 
Pia kila mwananchi nae atimize wajibu wake “It can be done play your part”.
Matarajio yetu ni kwamba leo tutapata mchango wa mawazo mbali mbali katika kubaliana na hali ya uchumi tuliyonayo sasa na kuishauri serikali njia nyingine za kukabiliana na changamoto hizi.
Kwa mara nyingine tena tunawakaribisha wote mliofika katika kongamano hili na tunaomba mtoe ushirikiano wa kuchangia mada mbali mbali zilizoandaliwa siku ya leo.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote walitusaidia kufanikisha kongamano hili ikiwa ni pamoja na taasisi zifuatazo:
1. African Barrick Gold Plc (ABG)
2. Car Track (T) Ltd
3. SIA Ltd (SME in Action)
4. Professional Approach Group
5. Mbezi Garden Hotel Ltd
6. Geo Fields (T) Ltd
7. New Solutions Inc. Ltd
8. ID Cards Solutions Ltd
9. www.gushit.com
10. Haak Neel Productions Ltd
Tunatoa shukrani za dhati pia kwa viongozi wote wa ndani na nje ya nchi walioweza kuja na kujumuika nasi leo hii.
Kuanzia leo tumezindua rasmi jukwaa la kiuchumi la kitaifa na tutalitumia jukwaa hili kila mara itakapobidi ili tupate kusikia maoni ya watanzania wote ambao hawana sauti ya kusema wakasika, sisi tutachukua mawazo hayo na kuyafikisha katika ngazi husika na pia tutamia jukwaa hili kama tanuru la kuibuwa fikra mpya za kimaendeleo. Kwa hiyo pale tutakapowaita tena mjitokeze kwa wingi.
Nawashukuru sana kwa kunisilikiliza, karibuni sana  na baada ya nasaha hizi napenda kutamka kuwa kongamano hili limefunguliwa rasmi.


No comments:

Post a Comment