Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma Frasser Kashai akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) Ofisini kwako.
Na.Pardon Mbwate na Felister, wa Jeshi la Polisi -Kigoma
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma leo limewafukuza kazi askari wake wanne kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya dola 300 za Kimarekani kutoka kwa raia mmoja wa China kinyume na maadili ya Jeshi hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma Frasser Kashai amewataja askari waliohukuzwa kazi kuwa ni mwenye namba E.3890 CPL Admirabils Malaso(43), G. 814 PC Waziri Juma Rashidi(30) G. 3012 PC Makasi Edwin(25) na G. 3322 PC Elias Zakaria(24) ambao wote walikuwa wakifanyia kazi katika kituo cha Polisi Uvinza wilaya ya Kigoma Vijijini.
Kamanda Kashai amesema kuwa mnamo Aprili 1, 2012 majira ya saa 5.00 usiku askari hao wakiwa zamu katika kituo hicho cha Polisi Uvinza, walipokea taarifa kwa njia ya simu ya mkononi kutoka kwa dada mmoja aitwaye Mary Kapele(26) akiwaeleza kuwa yuko katika nyumba moja ya kulala wageni ya Manchester na alikuwa na Raia wa Kichina mmoja wa wasimamizi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Kigoma Uvinza na kwamba waende kumshika ugoni ili wajipatie fedha na baadaye kugawana na dada huyo.
Askari hao walikwenda katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kumkamata Mchina huyo aitwaye Mafutao War, akiwa pamoja na dada huyo kisha wakamtaka atoe fedha kama malipo ya kumshika ugoni na ndipo walipopewa kiasi cha dola 300 za kimarekani na shilingi 10,000 za Kitanzania na kumuachia. Kamanda kashai amesema kuwa mlalamikaji Bw. War alikuwa ni mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya Chico inayojenga barabara ya kutoka Kigoma Uvinza.
Kamanda Kashai alisema baada ya kuona tukio hilo, raia wema walitoa taarifa Polisi mkoani Kigoma ambapo askari hao walikamatwa na baada ya uchunguzi kufanyika walibainika kuwa walihusika na tukio hilo na ndipo waliposhitakiwa kijeshi na kupatikana na hatia.
Amesema kufuatia hukumu hiyo ameamua kuwafukuza kazi kwa fedheha ili iwe fundisho kwa askari wengine kufuata utaratibu na sheria katika utendaji wa kazi zao za kila siku.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina.
No comments:
Post a Comment