Baadhi ya viongozi waliohudhuria uzinduzi wa kituo kipya cha macho kilichopo katika hospitali ya mkoa.
Kikundi cha uhamsishaji cha afya club kikitoa burudani kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha macho mjini Singida. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone ameuagiza uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida kuhakikisha watoto wa umri chini ya miaka mitano wenye matatizo ya macho, wanapelekwa haraka kwenye hospitali zenye huduma kwa watoto hao.
Dkt. Kone ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha upimaji wa macho (Vision centre), kilichopo katika hospitali ya rufaa ya mkoa mjini Singida.
Amesema kwa vile huduma hiyo haipatikani katika hospitali ya rufaa ya mkoa kwa watoto wenye umri huo ni muhimu watoto hao wakaharakishwa kupelekwa kwenye hospitali zenye uwezo wa kuwahudumia.
Dkt. Kone ametaja hospitali hizo kuwa ni pamoja na KCMC ya Moshi, hospitali ya taifa ya Muhimbili na CCBRT zote za jijini Dar es salaam.
Aidha, Dk. Kone ametumia fursa hiyo kuwashukuru wafadhili ambao wamekuwa wakitoa msaada wa nauli ya kwenda na kurudi kwenye hospitali hizo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano walio na matatizo ya macho.
“Ukizungumzia matatizo ya macho katika mkoa wetu wa Singida, huwezi kuacha kutaja jina la Mbunge wa Singida Mjini Mh. Mohammed Dewji kutokana na mchango wake mkubwa ambao ameendelea kuutoa kwa watu wanaokabiliwa na matatizo ya macho. Nachukua nafasi hii kumpongeza na namwomba aendeleze misaada hiyo kwa wakazi wa mkoa huu” amesema Dkt. Kone.
Awali mratibu wa taifa wa huduma za macho kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii Dkt. Nkunde Mwakyusa, amesema kuwa wizara kwa kushirkiana na wadau wa huduma za macho nchini, imeandaa mpango mkakati wa taifa wa miaka mitano wa huduma za macho nchini, ambao umeanza kutekelezwa Julai mwaka jana.
Amesema lengo la mpango mkakati huo, ni kuboresha utoaji wa huduma za macho hapa nchini kwa kuzingatia utatuzi wa changamoto zilizopo. Uboreshaji huo utafuata sera ya afya inayelekeza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika huduma ya afya.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwakyusa, Shirika lisilo la kiserikali la International Center for Eye Care Education (ICEE) limetoa msaada wa vifaa katika kituo hicho cha kutolea huduma ya macho ili kuboresha huduma.
Mganga wa macho mkoa wa Singida Dkt. Dismas Kimvule akitoa taarifa yake kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha macho mjini Singida.
Mwakilishi wa shirika la International Centre for Eye Care Education (ICEE) Afrika Mashariki Dkt. Naomi Nsubuga akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha macho.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha macho kilichopo katika hospitali ya mkoa mjini Singida. Kulia ni katibu tawala mkoa Liana Haasa na kushoto ni mganga mkuu wa mkoa Dkt. Doroth Kujugu.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akizindua rasmi kituo cha macho kilichopo kwenye hospital ya mkoa mjini Singida. Kulia ni Mwakilishi wa ICEE Naomi Nsubuga na wa kwanza kushoto ni Dkt. Nkunde Mwakyusa kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii.
No comments:
Post a Comment