Sunday, May 20, 2012

MAMA KIKWETE AHIMIZA USHIRIKIANO NA NGOS ZA MAREKANI KUINUA AFYA YA MTOTO NA MAMA.

 Mama Salma Kikwete kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Utawala wa Africa Diana White na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya Kimarekani wanaofanya kazi Tanzania kwenye masuala ya afya na lishe, baada ya mkutano wa pamoja tarehe 18-05-2012. 
 Mkuu wa Utawala wa Africare Bi. Diana White akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Africare nchini Tanzania kuanzia mwaka 1994 walipofungua ofisi zao nchini Tanzania kwenye Mkutano na Mama Salma Kikwete alipotembelea ofisi hizo tarehe 18-05-2012.
Mama Salma Kikwete akimkabidhi maelezo kuhusu WAMA Mkuu wa Utawala wa Africare Bi. Diana White kama ishara ya kuanzisha ushirikiano na taasisi hiyo ili kuendelea kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu masuala ya lishe Tanzania.








Washington DC
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewahimiza wadau afya na lishe kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na taasisi za Kitanzania na Serikali kwa ujumla ili kuinua afya ya mtoto na mama nchini Tanzania.
Aliyasema hayo alipokuwa kwenye mkutano wa pamoja na NGO sita za kimarekani zinazofanya kazi mbalimbali nchini Tanzania kwenye masuala ya lishe na afya tarehe 18 Mei 2012. Taasisi zilizohudhuria mkutano huo ni Malaria No More, Health Overseas Volunteers, Path International, Save the Children, Global Health and Diplomacy na Africare International, uliofanyika pembezoni na mikutano ya Rais Kikwete kuhusu masuala ya usalama wa chakula na lishe duniani.
Katika hotuba yake na taasisi hizo, Mama Salma Kikwete alizishukuru taasisi hizo kwa kufanya kazi Tanzania ili kusaidia taifa kufikia malengo yaliyowekwa kwenye dira ya taifa kuhusu masuala ya afya. Alihimiza ushirikiano na taasisi nyingine za Kitanzania hususan kwenye masuala ya uhamashaji, utoaji wa elimu na kujenga uwezo kwa Watanzania kwenye masuala ya lishe.
Akijibu swali la mtaalamu wa usalama wa chakula na lishe kutoka USAID Bi. Laura Birx, Mama Salma Kikwete alisema msaada mkubwa unaohitajika kwa Watanzania ni rasilimali fedha na elimu ili kuinua hali ya lishe kwa watoto wa Tanzania.
“Kwenye maeneo mengi mijini, elimu kuhusu lishe ni muhimu zaidi kwani baadhi ya familia wanauwezo wa kifedha na wanachohitaji sana ni elimu kuhusu lishe” Alisema Mama Kikwete.
Hii inatokana na hali ya maisha ya mjini ambapo wazazi wengi wanajikita na kazi na kuacha walezi wa nyumba kufuatilia lishe ya watoto. Alisema elimu kwa walezi hao ni muhimu sana ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanapewa lishe bora.
Hivi karibuni USAID kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali imetoa fedha $ 30 milioni kutekeleza mpango wa lishe Tanzania. Mpango huo ujulikanao kama Mwanzo BoraNutrition Program unatekelezwa kwenye mikoa mitatu ya Manyara, Morogoro na Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano. Mpango huo utakapokamilika utasaidia Serikali kujenga uwezo wa kutoa elimu kuhusu lishe, kuinua hali ya lishe ya watoto wadogo, wakina mama wajawazito na wanaonyonyesha. 
Mkutano wa Mama Salma Kikwete na taasisi hizo ulioratibiwa na Africare kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Marekani, umefungua milango ya ushirikiano baina ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na taasisi hizo sita ili kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa afya bora na lishe kwa watoto.
Kwenye ziara hiyo, Mama Kikwete na ujumbe wake pia walitembelea Hospitali Kuu ya Watoto Washington DC ya Children’s National Medical Center na kutembelea wodi ya watoto wenye mahitaji maalum. Wakati wa  ziara hiyo Mkurugenzi wa Hospitali hiyo kwenye masuala ya Uhusiano ya Kimataifa Dkt Jerome Paulson alikubaliana na Dkt Hadija Hemedi Mwamtemi, Mkuu wa Idara ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuanza mazungumzo ya kushirikiana kwenye kuelimisha walimu (Training of trainers) watakaofundishwa wengine kuhusu afya ya msingi kwa watoto ili kujikinga na magonjwa yatokanayo na uharibifu wa mazingira.
Dkt. Paulson alisema mpango huo wa kutoa elimu kwa watoa huduma ya afya kwa watoto hauna gharama kubwa lakini matunda yake yataonekana kwa kuwa na watoto wenye afya bora baada ya kuwalinda na magonjwa kama vile pumu yatokanayo na uchafuzi wa hewa.
Kwa upande wake Mama Salma Kikwete aliwasihi washirikiane na Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kwa pamoja kuanzisha mpango huo wa kubadilishana uzoefu na kupeana ujuzi (TOT) ili kulinda afya ya watoto wa Tanzania.
Mama Salma Kikwete alifanya ziara hiyo wakati Rais Kikwete akihudhuria Mkutano wa mwaka kuhusu Kilimo na Usalama wa Chakula Duniani Washington DC, Marekani.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania, Washington DC
19.05.2012


No comments:

Post a Comment