Monday, May 21, 2012

RAIS KIKWETE ATEUA MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua Majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani.
Walioteuliwa ni Jaji Semistodes S. Kaijage na Jaji Kipenka M. Musa na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Mei 21, 2012 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, uteuzi wao ulianza tokea Machi 15, mwaka huu, 2012.
Kabla ya kuteuliwa kwake kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kaijage (57) alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam tangu Mei 17, 2007. Aliteuliwa kuwa Jaji Mahakama Kuu Novemba 28, mwaka 2000.
Naye Jaji Musa (57) alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Pia amewahi kuwa Wakili wa Serikali, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba. Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Septemba 13, 2004.        
……..Mwisho………..

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Mei, 2012

No comments:

Post a Comment