Saturday, May 5, 2012

TWIGA STARS KUKIPIGA NA BONGO MOVIE TAIFA LEO.

Kikosi cha Timu ya Taifa wanawake Twiga Stars.
Mechi maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie sasa itachezwa leo (Mei 5 mwaka huu).
Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi hiyo, imerudishwa nyuma kwa siku moja kupisha mechi ya Yanga na Simba itakayochezwa Jumapili.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni ambapo viingilio kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu ni sh. 2,000, VIP C na B itakuwa sh. 5,000 wakati VIP A ni sh. 10,000.
Twiga Stars ambayo kwa sasa haina mdhamini na kambini katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani kujiandaa kwa mechi ya mashindano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia.
Timu hizo zitapambana Mei 26 mwaka huu  jijini Addis Ababa na kurudiana Juni 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mshindi atashiriki fainali za AWC zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).


No comments:

Post a Comment