Mkuu wa shule ya msingi ya Ikungi jimbo la Singida Mashariki akitoa taarifa yake ya kuanguka na kuzirai kwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo mbele ya mkutano mkuu maalum wa wazazi/walezi
Baadhi ya wazazi/walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi waliohudhuria mkutano mkuu maalum kujadili tatizo la kuanguka na kuzirai kwa wanafunzi. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu.
Busara za Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Singida Mzee Sumbu Galawa zimenusuru kuvunjika kwa mkutano maalum wa wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi Ikungi jimbo la Singida Mashariki.
Mkutano huo uliitishwa na uongozi wa shule hiyo na kamati yake, kwa ajili ya kujadili na kulitafutia ufumbuzi tatizo la baadhi ya wanafunzi kuanguka na kuzirai.
Dalili zilianza kujionyesha mapema kwamba mkutano huo usingemalizika salama, kutokana na kuwepo kwa kikundi ambacho kilidhamiria mwalimu mkuu wa shule hiyo Olvary Kamilly, anaondolewa katika shule hiyo.
Kiongozi wa Kikundi hicho kinachodaiwa ni cha wanachama wa CHADEMA Husseini Mwangia, kabla hata mwenyekiti wa kamati ya shule Naftali Gukwi hajafungua mkutano, alikuwa akilazimisha apewe nafasi ya kuzungumza.
Baada ya mwenyekiti Gukwi kufungua mkutano huo, alimruhusu Hussein Mwangia ambaye ilidaiwa kuwa hana mtoto anayesoma katika shule hiyo, kuzungumza.
Mwangia baada ya kuruhusiwa, huku akionyesha wazi kujawa na jaziba nyingi, alianza kutoa tuhuma mbali mbali kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo na mwenyekiti wa kamati.
Mwangia ambaye alichukua muda wa dakika 52 kuporomosha tuhuma hizo badala ya kuzungumzia mada pekee ya mkutano huo, alimtuhumu mwalimu mkuu kuwa hana ushirikiano na wazazi.
Aidha, alidai kuwa mwalimu huyo aliwahi kusema kuwa shule hiyo sio mali ya wazazi bali ni mali ya halmashauri ya wilaya ya Singida.
Baada ya mkutano huuo kuonyesha dalili za wazi kuwa amani na utulivu haipo tena wakati Mwangia akizungumza, mzee Galawa alipewa nafasi kutoa nasaha zake.
Mzee Galawa alisema kuwa jazba ikitawala mahalai po pote, huwa haijengi wala haitatui tatizo, bali hubomoa, kuongeza makali ya tatizo husika na mbaya zaidi, huchonganisha watu.
Kwa upande wake Jumanne Ngaa, yeye alipigilia msumari wa mwisho baada ya kusema kuwa wengi wa watu wanaoshinikiza mwalimu mkuu aondoloewe, hawana wanafunzi katika shule hiyo na kuwa lengo lao ni kutafuta umaarufu kwa siasa.
Baada ya maneno hayo, Mwangia alibaini kuwa upepo haupo tena upande wao,na hivyo aliwaamuru wanakikundi wenzake kususia mkutano huo na kuondoka mahali hapo.
Kabla ya kufungwa kwa mkutano huo, viongozi wa madhehebu ya dini za Kiislamu na Kikristo, walifanya sala ya kumwomba Mwenyezi Mungu, asaidie kuliondoa tatizo la kuanguka kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment