Thursday, June 14, 2012

HOTUBA YA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NDO HII

I   UTANGULIZI:

1.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liweze kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013.  Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinaelezea makisio ya mapato.   Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na Wakala wa Serikali; cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.

2.  Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3.         Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa mawaziri kama ifuatavyo: Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb); Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb); Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb); Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb). Aidha, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa naibu mawaziri katika Wizara mbalimbali, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb); Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb.); Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb.); Mhe.  January Yusuf Makamba (Mb.); Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb.); Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb.); Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb.); Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb.); na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb). Kadhalika, nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge.



4.         Mheshimiwa Spikanawapongeza pia, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa (Mb.); Mhe. Shy Rose Banji (Mb.); Mhe. Abdulah Alli Hassan Mwinyi (Mb); Mhe. Charles Makongoro Nyerere (Mb); Mhe. Dkt Twaha Issa Taslima (Mb); Mhe. Nderkindo Perpetua Kessy (Mb); Mhe. Bernard Musomi Murunyana (Mb); Mhe. Anjela Charles Kizigha (Mb.); Mhe. Maryam Ussi Yahaya (Mb.), ambao wamechaguliwa kutuwakilisha kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Ni matumaini yangu watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.

5.         Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Bajeti hii yamehusisha wadau na Taasisi mbalimbali. Napenda kuwashukuru walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho yake. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii. Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo yamezingatiwa katika Bajeti hii.

6.         Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa ushirikiano alionipatia wakati wa maandalizi ya Bajeti. Aidha, nawashukuru Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah; Naibu Katibu Wakuu, Ndugu Laston T. Msongole; Dkt. Servacius B. Likwelile; na Ndugu Elizabeth Nyambibo kwa mchango wao mkubwa katika matayarisho ya Bajeti. Vilevile, nawashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;         Dkt. Phillip Mpango, Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango; Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania; na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa. Nawashukuru wote kwa mchango wao katika maandalizi ya bajeti hii. Naishukuru pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.

7.         Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wao. Aidha, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Nawashukuru pia wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.


8.         Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mikutano ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Mwaka 2012 iliyofanyika kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 2 Juni 2012 na kufunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mikutano hii ilifanyika kwa ufanisi mkubwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 2,350 kutoka ndani na nje ya Tanzania. Hii imekuwa ni nafasi ya kipekee kwa Tanzania kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini. Aidha, washiriki wa ndani kutoka sekta binafsi walipata nafasi ya kufahamu fursa za mikopo zilizopo katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. Napenda kutoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa hizo kikamilifu.

9.         Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 imelenga kukabiliana na changamoto zinazokabili uchumi ikiwa ni pamoja na; kuongeza fursa za kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula nchini, kupambana na mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusimamia matumizi, kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.




II.  MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA     
   MWAKA 2011/12

10.       Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Mfumo wa Bajeti ya mwaka 2011/12 uliendeleza juhudi za Serikali za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, bajeti ilizingatia utekelezaji wa vipaumbele vya Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Mkakati wa Taifa wa Madeni; pamoja na kuimarisha usimamizi wa kodi na matumizi ya fedha za Umma.

11.       Mheshimiwa Spika,  misingi na shabaha za bajeti ya mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine, ililenga kukamilisha malengo ya Serikali ya kukabiliana na changamoto za kupunguza makali ya maisha kwa wananchi; kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani; kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje; kuendeleza sekta binafsi ili kupanua wigo wa kodi; kukamilisha maandalizi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa; na kutenga rasilimali na kutekeleza miradi katika maeneo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

12.       Mheshimiwa Spika, maeneo mengine yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya bajeti hiyo yalikuwa ni: kutekeleza mipango na mikakati maalum ya kuharakisha ukuaji wa uchumi; kutafuta mikopo ya masharti nafuu na ya kibiashara; kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya Binafsi ili kupanua fursa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo; Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012; kuhakikisha kwamba maduhuli ya Serikali yanakusanywa ipasavyo na kuwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali; pamoja na kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii, hususan elimu na afya ambazo zimekuwa na upanuzi mkubwa wa huduma.

Hatua za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12

Kupunguza Makali ya Maisha

13.       Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la kupunguza makali ya maisha kunakotokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: kurekebisha namna ya kukokotoa gharama za mafuta na kutangaza bei elekezi kila mwezi na kuanzisha utaratibu wa uagizaji mafuta kwa pamoja (bulk procurement). Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya upandaji wa bei ya mafuta hapa nchini.

14.       Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia shilingi bilioni 296 kutekeleza mpango wa dharura wa kukabiliana na tatizo la upungufu wa nishati ya umeme kwa kutumia mitambo ya kukodi. Utekelezaji wa jitihada hizi umeongeza megawati 324 kwenye Gridi ya Taifa. Kadhalika, Serikali ilitumia Dola za Marekani milioni 183 kugharamia ujenzi wa mitambo ya kufua umeme wa megawati 100 kwa mkoa wa Dar es Salaam mradi ambao umekamilika na uko kwenye hatua za majaribio na Megawati 60 kwa mkoa wa Mwanza ambao bado ujenzi unaendelea.

15.       Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia shilingi bilioni 27 kugharamia ununuzi na usambazaji wa tani 120,000 za mahindi katika masoko kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo. Aidha, Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya sukari. Kadhalika, Serikali ilipandisha kiwango cha riba inayotozwa na Benki Kuu kwa Taasisi za Fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58. Vilevile, Serikali ilipandisha kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinapaswa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.

Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira

 

16.       Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuongeza fursa za ajira. Hatua hizo ni pamoja na: kuboresha mazingira ya kisera na kisheria kuwezesha sekta binafsi kukua; kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp, na kufanikisha uanzishwaji wa kampuni ya kutoa mikopo ya muda mrefu ya ujenzi wa nyumba na makazi. Hatua nyingine zilizochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo, mawasiliano na kuwezesha wananchi kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kuna Taasisi mbalimbali ambazo zimechangia kutoa ajira kama vile, TASAF, SELF, VETA, Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Taasisi ndogondogo za Fedha, VICOBA, Benki za Kijamii na Mifuko ya Udhamini ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu. Katika mwaka 2011/12, Serikali iliajiri Walimu wa Shule za Sekondari na Msingi 25,000, Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo 4,499 na Watumishi wa Kada ya Afya 6,916.
 Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi

 

17.       Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji mwaka 2011 kufuatia kuidhinishwa kwake mwaka 2010. Kupitia Mpango huu, taratibu na kanuni za mawasilisho na malipo ya kodi na ushuru yanafanyika kwa njia ya mtandao. Utaratibu huu umeongeza ufanisi kwa kuondoa usumbufu na upotevu wa muda katika ulipaji wa kodi. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 75 ya walipa kodi wakubwa na walipa kodi wengine 2,795 wanafanya mawasilisho yao kwa njia ya mtandao.  Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha mfumo unaounganisha usimamizi wa kodi (Asycuda, ITAX) na benki za biashara ili kurahisisha ulipaji wa kodi.  Mfumo huu umeunganisha jumla ya benki 25.  Kadhalika, Mamlaka inatumia huduma za M-Pesa (Vodacom) na “NMB mobile” kwa ajili ya kulipia kodi ya majengo na kodi ya mapato.

 

 


18.       Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na jitihada za kupunguza urasimu katika utoaji wa mizigo bandarini kwa kuanzisha utaratibu wa kuwasilisha nyaraka kwa njia ya mtandao kabla ya mizigo kuwasili. Utaratibu huu umelenga kupunguza tatizo la mrundikano na upotevu wa nyaraka na kupelekea kupungua kwa muda na gharama za uagizaji na usafirishaji mizigo nje ya nchi.  Serikali imepunguza vizuizi vya usafirishaji mizigo ndani ya nchi kutoka 50 vilivyokuwepo kufikia 15, isipokuwa vituo vya mizani na forodha. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za kufanya biashara na usumbufu wanaopata wafanyabiashara.

Sera za Mapato

 

19.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi kwa kuchukua hatua za kiutawala, kisera pamoja na marekebisho ya viwango vya kodi na sheria.

20.       Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ili kuboresha uzalishaji katika sekta za Kilimo, Mifugo, Viwanda, Biashara na Utalii. Marekebisho hayo ni pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vipuri vya zana za kilimo; chakula cha kukuzia kuku; nyuzi za kutengenezea nyavu za kuvulia samaki; pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwarejeshea kodi wageni kwa bidhaa walizonunua nchini wakati wanaondoka.

21.       Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kuuza na kupangisha majengo ya nyumba za kuishi za Shirika la Nyumba la Taifa - NHC; kuondoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali isipokuwa kwenye vifaa vya misaada kwa vituo vya kulelea watoto yatima na shule.

22.       Mheshimiwa Spika, Serikali pia ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa kufuta kodi ya Zuio kwa usafirishaji wa samaki nje ya nchi ili kuongeza utoaji wa huduma za usafirishaji wa mazao ya samaki kutokea hapa nchini badala ya kupitia nchi za jirani. Aidha, marekebisho yalifanyika katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ili kupunguza gharama za uzalishaji.

23.       Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA 220 ilifanyiwa marekebisho kwa kutoa msamaha wa ushuru unaotozwa kwenye mafuta yanayotumika katika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili kupunguza gharama. Aidha, marekebisho yalifanyika kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004 kufuatia  kuridhia kwa Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama kufanya marekebisho mbalimbali katika kukuza Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Mifugo, Biashara na Utalii. Vilevile, marekebisho yalilenga katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.



24.       Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha na kuhakikisha mashine za kielectroniki – EFD zinatumika ipasavyo; kuimarisha mfumo wa kusimamia vitalu vya kodi; kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa wateja na vya kukusanyia mapato; kuimarisha mifumo ya malipo ya kodi; na kuboresha mfumo wa uthaminishaji kwa kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi.

Mwenendo wa Ukusanyaji Mapato

25.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya shilingi bilioni 13,525.9 kutoka katika vyanzo mbalimbali na kutumia kiasi hicho kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Vyanzo vya mapato vilikuwa kama ifuatavyo: mapato ya ndani yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 6,775.9; mapato kutoka Serikali za mitaa yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 350.5; misaada na mikopo ya kibajeti ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 869.4; misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na ya kisekta ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 3,054.1; mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1,664.9; na mikopo ya kulipia dhamana na hatifungani zinazoiva zilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 810.9.

26.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri, hadi Aprili 2012 makusanyo yamefikia jumla shilingi bilioni 5,684.5. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 80 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 7,126.4 kwa mwaka 2011/12.

27.       Mheshimiwa Spika, makusanyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 5,227.5 ambayo ni sawa na asilimia 84 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 6,228.8. Kulingana na mwenendo wa makusanyo ya mapato ya kodi kwa kipindi cha miezi kumi ya mwaka 2011/12, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2011/12 Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 6,307.8 na hivyo kuweza kufikia lengo tulilojiwekea.


28.       Mheshimiwa Spika, mapato yasiyotokana na kodi yamefikia shilingi bilioni 451.6 ikiwa ni asilimia 83 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 547.1 kwa mwaka. Kutokana na mwenendo huo, Serikali inatarajia hadi Juni 2012 kufikia lengo.

 29.      Mheshimiwa Spika, mapato ya Serikali za Mitaa yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 143, sawa na asilimia 40.8 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 350.5 kwa mwaka. Hadi Juni 2012, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200 kutokana na chanzo hiki ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la mwaka. Kutokufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato haya kumechangiwa na kuchelewa kuanza kutekeleza utozaji wa ada za leseni.

Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu Kutoka Nje

30.       Mheshimiwa Spikakatika mwaka 2011/12, Serikali ilikadiria kupata kiasi cha shilingi bilioni 869.4 kama misaada na mikopo ya kibajeti ambapo hadi sasa Serikali imepokea shilingi bilioni 916.3, ikiwa zaidi kwa shilingi bilioni 46.9. Ongezeko hili limetokana na baadhi ya wafadhili kutoa fedha zaidi ya kiwango walichoahidi. Kwa upande wa misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta, hadi kufikia Aprili 2012 ilifikia shilingi bilioni 1,450.4 sawa na asilimia 47 ya makadirio ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 3,054.1. Upungufu huu umesababishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi na kuchelewa kupokea taarifa ya fedha hizi kutoka kwa washirika wa maendeleo na Wizara na Taasisi zinazotekeleza miradi husika.

Mikopo ya Ndani

31.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali imekopa kiasi cha shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ikiwa ni asilimia 64 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 819.1. Aidha, Serikali ilipanga kukopa shilingi bilioni 393.4 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2012, Serikali ilikuwa imekopa shilingi bilioni 232.6 sawa na asilimia 59 ya makadirio ya mwaka.
Mikopo ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara

32.       Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12 Serikali ilikadiria kukopa kiasi cha Dola za Marekani milioni 822, sawa na shilingi bilioni 1,271.6 kama mikopo ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 310 na Benki ya Standard ya Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili 2012, jumla ya Dola za Marekani milioni 229 ambazo zilitumika kulipia madeni ya barabara ya mwaka 2010/11. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa Euro milioni 61 na Benki ya HSBC. Mkopo huu umeelekezwa kugharamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato Mwanza. Serikali pia imesaini mkataba wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 350 kutoka Benki ya Credit Suisse ya Uingereza ambapo Dola za Marekani milioni 200 zimepokelewa mwanzoni mwa Mwezi Juni 2012. Kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 150 kitapatikana na  kutumika mwaka 2012/13.


33.       Mheshimiwa Spika, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi ambaye ataishauri Serikali katika zoezi la kujiandaa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (Sovereign Credit Rating). Maandalizi haya yataiwezesha nchi kufanyiwa tathmini yanatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2013. Kukamilika kwa zoezi hilo kutawapatia wakopeshaji imani na hivyo kuiwezesha Serikali kupata mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara kwa wakati.

Sera za Matumizi

34.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kutekeleza sera za matumizi kulingana na upatikanaji wa mapato ya ndani, misaada pamoja na mikopo ya ndani na nje. Aidha, Serikali iliendelea kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, ikijumuisha udhibiti wa ulipaji wa mishahara, matumizi katika miradi ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo, ununuzi wa umma na kuendelea kudhibiti malimbikizo ya madeni. Serikali imeandaa mkakati wa kulipa na kudhibiti madeni yatokanayo na malimbikizo ya madai ya watumishi; wakandarasi; wazabuni; na madeni mengineyo. Madeni hayo yatalipwa baada ya kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.

Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma

35.       Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, Serikali iliendelea kutekeleza programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Serikali za mitaa. Katika utekelezaji wa programu hiyo Serikali imeweka mtandao wa IFMS katika Halmashauri 133. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo ya kibenki - TISS kwa watumishi wa kada ya Uhasibu katika mikoa 20, Hazina ndogo zote, Ofisi ya Bunge, TAMISEMI na Ofisi ya Mrajisi wa vyama vya Ushirika.  Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa Wahasibu wa Wizara, Idara, Mikoa na Balozi zetu 32 katika kuandaa Hesabu za Serikali kwa viwango vya Kimataifa (IPSAS – Accruals basis).

36.       Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho hayo, usimamizi wa fedha katika Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa unaendelea kuimarika. Hali hii inajidhiirisha katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/11 ambapo Hati safi za ukaguzi kwa Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa zimeongezeka kutoka asilimia 71 hadi asilimia 85. Wakati Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 26 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 15 kwa mwaka wa fedha 2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha ikilinganishwa na mwaka 2009/10 ambapo Hati hizo zilitolewa kwa Taasisi mbili.

37.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Balozi zetu Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 85 mwaka 2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha katika mwaka 2010/11.  Aidha, kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 54 mwaka 2010/11 na Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 64 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 56 mwaka 2010/11.
 38.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali imefungua akaunti sita kwa kila Halmashauri kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu yao. Akaunti hizo ni za Mapato; Amana; Matumizi ya kawaida; Mishahara; Maendeleo; na Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uendeshaji, urasimu wa matumizi, ugumu wa kutoa taarifa za matumizi, ulimbikizaji wa fedha kwenye akaunti bila kutumika kwa muda mrefu na kudhibiti fedha zisitumike katika shughuli ambazo hazikuidhinishwa.

Mwenendo wa Matumizi

39.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali ilikadiria kutumia kiasi cha shilingi bilioni 13,525.9 katika mwaka wa fedha wa 2011/12. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo; kiasi cha shilingi bilioni 8,600.3 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,925.6 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Matumizi ya kawaida

40.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012 matumizi ya kawaida yamefikia shilingi bilioni 7,349.8 sawa na asilimia 85.5 ya makadirio ya mwaka kama ilivyo katika ridhaa ya matumizi. Kati ya kiasi hicho, malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma yalikuwa shilingi bilioni 2,760.5 sawa na asilimia 84.4 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 3,270.3. Malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 316.1 sawa na asilimia 102.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 308.7 kwa mwaka. Malipo ya mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 57.3 sawa na asilimia 85.7 ya makadirio kwa mwaka. Serikali ilitumia shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba.


41.       Mheshimiwa Spika, matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 2,384.9 ikiwa ni asilimia 72.8 ya makadirio ya shilingi bilioni 3,275.1 kwa mwaka. Kati ya matumizi mengineyo, kiasi cha shilingi bilioni 284.1 zilitumika kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa ni asilimia 89 ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 317.4, na hivyo kunufaisha jumla ya wanafunzi 93,176. Kadhalika, Serikali ililipa kiasi cha shilingi bilioni 44.0 za madai ya walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyohakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.

Matumizi ya Maendeleo

42.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 2,657.2 ziligharamia miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni 4,924.6. Fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 1,201.6 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 1,871.5 sawa na asilimia 64.2. Upungufu huu umetokana na kuchelewa kupatikana kwa wakati kwa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara. Jumla ya shilingi bilioni 663.8 ziligharamia miradi ya miundombinu, kati ya hizo shilingi bilioni 296 zilitumika kwenye miradi ya umeme na shilingi bilioni 367.8 kwenye miradi ya barabara. Matumizi ya maendeleo yaliyogharamiwa kwa fedha za nje yalikuwa shilingi bilioni 1,450.4 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 3,054.1 sawa na asilimia 47.

Vitambulisho vya Taifa na Anwani za Makazi

43.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na azma yake ya kutekeleza mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia, pamoja na mambo mengine, kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za kifedha. Mradi huu unaenda sambamba na uanzishwaji wa anwani za makazi. Vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa katika robo ya kwanza ya mwaka 2012/13 kwa Zanzibar na Mkoa wa Dar es Salaam.


Sensa ya Watu na Makazi na Utafiti Kuhusu Hali ya Umaskini

44.       Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi Serikali imeendelea kugharamia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95. Hadi sasa Serikali imetumia shilingi bilioni 23.6 kugharamia maandalizi ya zoezi la Sensa. Sensa hiyo imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti 2012. Aidha, Serikali iliendelea kugharamia utafiti wa mapato na matumizi katika kaya. Utafiti huu ulianza mwezi Oktoba 2011, na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2012 na matokeo yanatarajiwa kutoka mwezi Julai 2013. Utafiti huu utatoa picha halisi ya hali ya umaskini, hususan wa kipato tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2012. Hii itasaidia kutambua mwenendo wa umaskini wa kipato na sababu zilizopelekea mwenendo huo.



Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)

45.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/12, serikali iliendelea kutekeleza MKUKUTA awamu ya pili unaojielekeza katika maeneo ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, kuboresha maisha na ustawi wa jamii, na utawala bora na uwajibikaji sambamba na Melengo ya Maendeleo ya Milenia. Ili kufikia matokeo tarajiwa katika kila eneo, sekta kadhaa huchangia katika utekelezaji kupitia sera, mikakati na mipango ya kisekta. Kwa mantiki hiyo, utekelezaji wa MKUKUTA II unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali za uchumi katika hatua ya upangaji na utekelezaji.

46.       Mheshimiwa Spika, MKUKUTA ni mkakati unaoziweka pamoja juhudi za Serikali na wadau mbalimbali katika kupambana na umaskini. Aidha, umaskini ni suala pana linalojumuisha umaskini wa kipato na usio wa kipato. Ni kweli kuwa umaskini wa kipato umekuwa ukipungua kwa kasi ndogo. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kupunguza umaskini kwa kujenga mazingira bora ili wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu, afya, miundombinu na sekta ya fedha.

47.       Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto zilizojitokeza, hususan mtikisiko wa uchumi duniani, uchumi uliendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2011, kilikuwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010. Aidha, pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi 770,464 kwa mwaka 2010 hadi shilingi 869,436 kwa mwaka 2011. Kwa wastani, ongezeko hili limeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na nyumba bora, simu za mkononi, pikipiki na usafiri wa baiskeli.

48.       Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza programu mbalimbali za huduma ya jamii kwa lengo la kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Matokeo ya utekelezaji wa programu hizo zinaonesha mabadiliko chanya. Katika sekta ya elimu, viwango vya uandikishaji na kumaliza katika ngazi zote za elimu vinaridhisha. Mfano, kiwango cha uandikishwaji katika elimu ya msingi, kilikuwa asilimia 94 na katika elimu ya sekondari ni asilimia 35 kwa mwaka 2011. Huduma za afya kwa mtoto na mama zinaendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa mpango wa afya ya mtoto na mama. Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa programu ya sekta ya maji iliyoanza mwaka 2007.

49.       Mheshimiwa Spika, katika kudumisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha sekta ya sheria kwa kuongeza idadi ya mahakimu wa Mahakama za mwanzo; kuimarisha mfumo wa sheria na haki za binadamu; kuhamasisha umma kuhusu haki za binadamu na wajibu wa jamii; na kushiriki katika mpango wa nchi za Afrika kujitathmini zenyewe katika masuala ya utawala bora. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma, kwa kuimarisha ofisi za ukaguzi katika wizara, mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Sekta ya Fedha

50.       Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mageuzi mbalimbali katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba inachangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Mageuzi haya yameleta mafanikio makubwa.Hadi kufika mwezi Aprili mwaka 2012 idadi ya benki imeongezeka na kufikia 49 kutoka benki 43  Aprili mwaka 2011. Kadi za simu za mkononi zinazotumika kutoa huduma za kifedha zimefikia 21,184,808 mwaka 2011 kutoka 10,663,623 mwaka 2010. Aidha, idadi ya Taasisi ndogo ndogo za kifedha  zimefikia 150 mwaka 2011.

51.       Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutoa Mikopo ya kilimo kupitia dirisha la Kilimo lililopo katika Benki ya Rasilimali Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya mikopo 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 22.9 ilitolewa, kati ya mikopo hiyo, 42 ni ya SACCOS, 32 ni kwa ajili ya makampuni na 7 kwa Taasisi ndogondogo za fedha (MFIs). Mikopo iliyotolewa kwa MFIs na SACCOS ilitumika kukopesha miradi mingi ya wakulima wadogo wadogo vijijini. Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya mtaji wa Benki ya Kilimo.

52.       Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na utekelezaji wa programu ya mageuzi na maboresho ya Ushirika nchini ili kuimarisha vyama vikuu vya ushirika na kuviwezesha kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi hususan waliopo vijijini. Mwaka 2011, idadi ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) iliongezeka na kufikia 5,346 kutoka vyama 5,314 mwaka 2010. Vile vile, idadi ya wanachama iliongezeka kwa asilimia 5.7 na kufikia wanachama 970,655 kutoka wanachama 917,889 mwaka 2010. Aidha, Hisa, Akiba na Amana za wanachama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 236.8 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 399.0 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 68.5. Mikopo iliyotolewa kwa wanachama iliongezeka kutoka shilingi bilioni 539.2 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 627.2 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 16.3. 


53.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 21.9 ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi 2011. Ongezeko hili linaenda sambamba na kuongezeka kwa rasilimali za fedha za ndani kwenye benki pamoja na kupungua kwa ukuaji wa rasilimali za fedha za kigeni kwenye benki. Sehemu kubwa ya mikopo hii ilielekezwa katika shughuli binafsi asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9; uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na usafiri na mawasiliano asilimia 7.9.

54.       Mheshimiwa Spika, ili kuongeza upatikanaji wa mikopo, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kuanzisha taasisi ya kuratibu taarifa za wakopaji (Credit Rerefence Bureau) na mfumo wa kuhifadhi taarifa za wakopaji (Credit Reference Databank). Mshauri mwelekezi ameanza zoezi la kuweka mitambo na kutoa mafunzo kwa watumiaji. Aidha, Serikali imeboresha mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na kati kwa ajili ya nyumba, Kilimo na uwekezaji ambapo kanuni za  taasisi za fedha za maendeleo ziliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la Machi 2012.
55.       Mheshimiwa Spikakatika mwaka 2011/12, Serikali imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kufanya tathmini ya uwekezaji wa mifuko, uhai wa mifuko, pamoja na kuandaa mwongozo za uwekezaji wa mifuko hiyo. Aidha, Serikali imefanya marekebisho ya Sheria za Mifuko yote pamoja na Mamlaka ya Usimamiaji wa Shughuli za Mifuko (SSRA) ili kuboresha usimamizi wa mifuko hiyo.

Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi

56.       Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lilipitisha sheria mpya ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2010 ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa miundombinu na kuiendesha kwa lengo la kutoa huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa wananchi. Katika mwaka 2011/12, Serikali imefanya maandalizi ya utekelezaji wa Sera ya Ubia ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya PPP kwa kila Wizara na kuandaa miongozo itakayotumika kuchambua na kuidhinisha miradi ya Ubia kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeanza hatua za awali kubaini miradi inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa Ubia kwa mujibu wa sheria.
57.       Mheshimiwa Spika, dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inatekelezwa kwa kutumia sheria mbili – Sheria ya Ubia ya mwaka 2010 na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 iliyorekebishwa mwaka 2011. Sababu za kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na mambo mengine ni kuingiza vifungu vinavyowezesha Taasisi za Serikali kupata Wabia makini wa uwekezaji katika miradi ya Umma kwa njia zilizo wazi. Aidha, katika mwaka 2012/13, Serikali itakamilisha Kanuni za Sheria ya Ununuzi wa Umma ambazo zinazingatia mazingira ya kipekee ya Sheria ya Ubia ambayo inawezesha kupata Wabia walio tayari kuwekeza katika miradi husika. Serikali itahakikisha kanuni na taratibu zote za kuidhinisha na kusimamia miradi ya ubia zinazingatiwa.

58.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali itatoa mafunzo ya uelewa wa dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi kwa watumishi wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi za Serikali, na Halmashauri zote. Aidha, Serikali itachagua miradi michache ya kuanza nayo ili kupata uzoefu wa uendeshaji wa miradi hiyo. Maeneo tunayotarajia kuanza nayo ni barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, maji pamoja na ujenzi wa ofisi.

59.       Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia fursa hii kuziomba Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhamasisha Sekta Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria.

Usimamizi wa Deni la Taifa

60.       Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma yake ya kuboresha miundombinu ya kimkakati, Serikali imeendelea kukopa kutoka nje na ndani ya nchi ili kugharamia miradi mbali mbali ya maendeleo. Hadi mwishoni mwa Machi 2012, deni la taifa lilikuwa shilingi bilioni 20,276.6 ikilinganishwa na deni la shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 15.4. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15.306.9 zilikuwa ni deni la nje na shilingi bilioni 4,969.7 ni deni la ndani.  Kati ya kiasi cha deni la nje, shilingi bilioni 12,342.5 zilikuwa ni deni la umma na kiasi kilichobaki cha shilingi bilioni 2,964.4 ni deni la sekta binafsi. Aidha, hadi kufikia Machi 2012, deni la ndani la Serikali lilifikia shilingi bilioni 4,969.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,496.5 mwezi Machi, 2011, sawa na ongezeko la asilimia 10.5. Sababu kubwa ya kuongezeka kwa deni la taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na utumiaji wa dhamana za muda mfupi za Serikali kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei katika uchumi na kushuka kwa thamani ya shilingi kuliongeza deni la nje.

61.       Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa vizuri, mwezi Februari, 2012, Serikali ilifanya tathmini ya uhimilivu wa deni (Debt Sustainability Analysis) likijumuisha dhamana zinazotolewa na Serikali kwa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma ambapo matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa Deni la Taifa linahimilika.

Usimamizi wa Mashirika ya Umma

62.       Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Taasisi, Wakala na Mashirika ya umma yanatekeleza majukumu yao, Serikali imetoa Waraka Na.1 wa mwaka 2012 unaoelekeza Wizara mama na Bodi za Wakurugenzi kuingia katika mikataba ya utendaji, Waraka huo umeanza kutumika Januari, 2012. Aidha, ukaguzi wa kiutendaji (Management Audit) katika Taasisi za Serikali umefanyika kwa baadhi ya Taasisi na Mashirika ya umma kwa kuangalia uzingatiaji wa kanuni, Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja na uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya fedha na  taratibu za ajira. Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuboresha uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Serikali. Kadhalika, Serikali imefanya uhakiki wa mashirika 170 yaliyobinafsishwa. Kati ya hayo, mashirika 41 yalikutwa yanajiendesha kwa faida, mashirika 66 yanajiendesha kwa hasara na mashirika 63 yalikuwa muflisi. Kwa yale ambayo yanaendeshwa kwa hasara yatawekwa chini ya mfilisi kwa lengo la kuyachambua na kupendekeza hatua za kuchuliwa. Aidha, kwa yale yaliyokuwa muflisi hatua za kuyafilisi zinaendelea.




III.  BAJETI YA MWAKA 2012/13

63.       Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na program za maboresho katika sekta ya umma.  Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

64.       Mheshimiwa Spika, pamoja na miongozo hiyo, Bajeti hii inazingatia pia changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika; kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la Dunia; uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo; kupanda kwa bei za bidhaa na huduma; kutopatikana kwa wakati fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kulikosababishwa na masharti magumu na urasimu kwa mikopo ya kibiashara; na kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani, hususan ya wazabuni, wakandarasi na watumishi. Mambo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na mwenendo wa uchumi wa dunia na makubaliano ya kikanda na kimataifa. Serikali imepanga hatua mbalimbali za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo kama nitakavyoeleza hapo baadae.

Shabaha na Malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13

65.       Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13, imejielekeza katika kufikia Shabaha na malengo yafuatayo:

                      i.        Kukuza Pato halisi la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011;

                     ii.        Kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha  umeme, barabara, reli na bandari;

                    iii.        Kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha;

                    iv.        Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia  18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12;

                     v.        Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja;

                    vi.        Kuwa na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha;

                   vii.        Kukua kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la Taifa mwishoni mwa Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei;

                  viii.        Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne na nusu;
                    ix.        Kuimarisha utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kupanua fursa za kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;

                     x.        Kuboresha mazingira ya wafanya biashara wadogo na wakati;

                    xi.        Kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;

                   xii.        Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na

                  xiii.        Kujenga uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.

                 



                  Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka 2012/13

66.       Mheshimiwa Spika; ili kufikia malengo yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ni hii ifuatayo:

                      i.        Kuendelea kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii;

                     ii.        Kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;

                    iii.        Kuimarika kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti;

                    iv.        Kuendelea kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo;

                     v.        Kuendelea kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi;

                    vi.        Kuendelea kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma;na

                   vii.        Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za uwekezaji.
                 
                  Sera za Mapato

67.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi na yasiyotokana na kodi; na kupanua wigo wa makusanyo. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia kwa kiwango kikubwa matumizi ya kawaida kwa kutumia mapato ya ndani. Sera za mapato zitakazozingatiwa kwenye Bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na;

                      i.        kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa mapato yasiyo ya kodi kwa kupitia upya mfumo wa utoaji stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;

                     ii.        kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;

                    iii.        kuendelea kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;

                    iv.        kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la  kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;

                     v.        Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
                    vi.        kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na

                   vii.        Kujenga uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya madini, gesi na petroli.

Hatua za Kuboresha Uzalishaji na Huduma

68.       Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waheshimiwa wabunge kuhusu haja ya kuboresha mazingira ya uzalishaji katika sekta za Uvuvi, Viwanda, Kilimo, Mifugo na Utalii. Hatua ambazo Serikali imepanga kuchukuwa ni pamoja na:



                      i.        Kupitia upya vivutio kwa sekta ya viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za ndani vikiwemo viwanda vya nguo na mafuta ya kula;

                     ii.        Kutafuta utaratibu mzuri wa kubainisha vipuri vya mashine na mitambo inayosamehewa kodi ili kuondoa usumbufu wanaoupata waagizaji;

                    iii.        Kupitia upya viwango vya kodi katika sekta ya Kilimo na Uvuvi kwa lengo la kuviwianisha na kupunguzwa;

                    iv.        Kupitia upya maudhui na viwango vya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Skills Development Levy) na Leseni ya Magari (Motor Vehicle Licence). Kwa kufanya hivyo, Serikali inalenga katika kupanua wigo wa kodi, kuwapunguzia mzigo waajiri na kupanua ajira hapa nchini. Aidha, mapitio ya Leseni za Magari yatazingatia kurejea madhumuni ya kuanzishwa kwa leseni hiyo; na

                     v.        Kufanya mapitio ya Sheria ya VAT kwa lengo la kuibadili kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa “Best Practice”.

69.       Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuzingatia fursa zilizopo. Aidha, OWM – TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Misaada na Utaalamu la Ujerumani – GIZ watakamilisha na kusambaza kwenye Halmashauri mfumo wa kompyuta wa utunzaji kumbukumbu za mali na majengo (Integrated Property Rating Information Management System - IPRIMS) ili kuboresha ukusanyaji wa mapato hususan kodi ya majengo. Natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuweka msukumo utakaowezesha Halmashauri kukusanya kikamilifu kodi ya majengo pamoja na mapato mengine ili kuziongezea uwezo wa kuhudumia wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.


70.       Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za mapato zilizoainishwa hapo juu, Serikali inalenga kukusanya mapato ya ndani (bila kujumuisha Halmashauri) shilingi bilioni 8,714.7 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa. Kati ya kiwango hicho, mapato ya kodi shilingi bilioni 7,080.1 na mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 644.6. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.

Mikopo ya Ndani

71.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kukopa katika soko la ndani la fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva. Katika mwaka 2012/13, Serikali inakusudia kukopa kiasi cha shilingi bilioni 1,632 kutoka soko la fedha la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 483.9 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva. Kiwango hiki kimezingatia viashiria vya kiuchumi pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zinaendelea kutoa mikopo kwa Sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Misaada na Mikopo Mipya yenye Masharti Nafuu

72.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha Misaada na mikopo inapatikana kwa wakati na kuchangia katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Katika bajeti ya mwaka 2012/13 serikali inatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni 3,156.7 kutokana na misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Kati ya fedha hizo, Misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 842, sawa na Dola za Marekani milioni 495. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2,314.2.


73.       Mheshimiwa Spika, pamoja na misukosuko ya kiuchumi na majanga ya kiasili iliyozikumba nchi Wahisani, bado zimeendelea kutoa misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwatambua washirika wetu wa maendeleo ambao ni: Uingereza, Norway, Canada, Marekani, Uholanzi, Ubelgiji, China, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Japani, Korea ya Kusini, Denmark, Hispania, Sweden, Uswisi, India, Italia, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, Global Funds, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), BADEA, Kuwait Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi Fund, na Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru Sana.

Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara

74.       Mheshimiwa Spika, sera ya Serikali ni kutafuta mikopo nafuu kutoka mashirika na nchi wahisani kwa ajili ya kugharamia Bajeti yake ya maendeleo. Hata hivyo, kwa kuzingaita mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu kwa mwaka 2012/13, Serikali inatarajia kupata kutoka nje mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi cha shilingi bilioni 1,254.1 sawa na Dola za Marekani milioni 749. Fedha hizi zitatumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ikijumuisha  mchango wa Serikali (counterpart fund) katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa maji wa Ruvu chini na ujenzi wa barabara. Uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la Taifa uliopo.

Sera za Matumizi

75.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, sera za matumizi zitazingatia yafuatayo:
                      i.        Matumizi yataendelea kuzingatia mapato halisi yanayopatikana;

                     ii.        Nakisi ya bajeti haitazidi asilimia 5.5 ya Pato la Taifa, ikijumuisha ruzuku;
                    iii.        Mafungu yataendea kuzingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;

                    iv.        Maafisa Masuuli wataendelea kuzingatia Sheria ya Fedha na ya Ununuzi wa Umma; na

                     v.        Serikali inaendelea kukusanya madeni yote kwa lengo la kuyahakiki na kuyapangia utaratibu wa kuyalipa.

Matumizi ya Kawaida

76.       Mheshimiwa Spika, Sera za matumizi ya kawaida kwa mwaka 2012/13 zinalenga pamoja na mambo mengine katika kugharamia mishahara; madeni ya mikopo ya ndani na nje; uboreshaji wa huduma za kiuchumi na maendeleo ya jamii; mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; mitihani ya shule za msingi na sekondari; ununuzi na usambazaji wa dawa; mahitaji ya Tume ya Kuratibu Mabadiliko ya Katiba; matengenezo ya mali ya Serikali; ununuzi wa chakula cha hifadhi; mahitaji ya kawaida kwenye miradi iliyokamilika; pamoja na kuendelea kulipa madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni.
77.       Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu, kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira, Serikali imetenga fedha katika maeneo yafuatayo:  Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Benki ya Rasilimali; shilingi bilioni 40 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na hivyo kufikisha mtaji wa shilingi bilioni 100. Aidha, shilingi bilioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, ambapo katika awamu ya kwanza vijana 5,000 wanatarajiwa kujiunga. Vilevile, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 70.7 katika maeneo mapya ikiwa ni Mikoa, Wilaya na Halmashauri kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo.

Matumizi ya Maendeleo

78.       Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen Masatu Wasira, aliainisha miradi ya kitaifa ya kimkakati pamoja na miradi katika maeneo muhimu ya ukuaji wa uchumi. Bajeti hii itazingatia vipaumbele hivyo:

a)    Miundombinu
                      i.        umeme - mkazo utawekwa katika upatikanaji wa umeme wa kuhakika kwa kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji ambapo jumla shilingi bilioni 498.9  zimetengwa kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.

                     ii.        usafirishaji na uchukuzi – uimarishaji wa reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni. Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya shilingi bilioni 1,382.9 zimetengwa katika eneo hili.
iii          maji  safi na salama -  kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama mijini na vijijini. Kiasi cha shilingi bilioni 568.8 kimetengwa.

iv          Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
– kuimarisha mawasiliano kwa kutumia TEHAMA ili kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa taarifa za  masoko ya ndani na nje ya nchi; ukusanyaji wa mapato; huduma za afya; elimu; huduma za kifedha; n.k. Jumla ya shilingi bilioni 4 zimetengwa katika eneo hili.

b)    Kilimo, Uvuvi na Ufugaji

79.       Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa kilimo na kukuza kilimo cha misitu.  Hii ni pamoja na kuendeleza shughuli za ufugaji na uvuvi ili ziwe na tija kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji; kwa kufanya hivyo kutapunguza umaskini wa kipato.
80.       Mheshimiwa Spika, katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, Serikali itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha kwamba nguzo zake zote zinaendelea kuzingatiwa; kuhakikisha kwamba walengwa wanapata pembejeo kwa wakati; Maafisa ugani kutakiwa kuwa na mashamba yao ya mfano (mashamba darasa) ili kuwaelimisha wakulima kilimo cha kisasa; kuongeza msukumo kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya shughuli zao za kilimo katika misimu yote badala ya kutegemea mvua;Kuimarisha masoko ya mazao kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo imeshaanza shughuli zake; na Mikoa kutakiwa kuendelea  kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje. Kiasi cha shilingi bilioni 192.2 kimetengwa katika eneo hili.





c)     Maendeleo ya Viwanda

81.       Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji; na viwanda vya eletroniki na TEHAMA pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Hatua hii inaenda sambamba na kuboresha na kuimarisha viwanda vidogo vidogo nchini. Jumla ya shilingi bilioni 128.4 zimetengwa katika eneo hili.

d)    Maendeleo ya Rasilimali Watu na Huduma za Jamii

82.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imepanga kuboresha viwango vya elimu katika ngazi zote hususan katika maeneo ya utafiti, ufundi stadi, afya; sayansi na ujuzi maalum kuhusu madini, gesi, urani, chuma na mafuta; hatua hii inajumuisha ukarabati wa maabara na upatikanaji wa vifaa vya maabara. Shilingi bilioni 84.1 zimetengwa katika eneo hili.

e)    Utalii

83.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma zitolewazo katika eneo hili ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii na kuboresha mazingira ya kitalii na kutoa mafunzo ya utalii, kuainisha maeneo mapya ya utalii na kuboresha vyuo vya utalii.

Huduma za Fedha

84.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kifedha hususan mifumo ya kuweka akiba na kukopa kama vile SACCOS, VICOBA na benki za kijamii ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uzalishaji. Kiasi cha shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa Benki ya Wanawake, Mradi wa SELF na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Aidha, Wizara ya Fedha itaendelea kusimamia maendeleo ya Taasisi za fedha zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali. Ili kufanikisha hili kitengo kilichopo cha maendeleo ya sekta ya fedha kitahuishwa na kuwa idara kamili.
Usimamizi wa Fedha za Umma
                                                                                        
85.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya nne ya Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma na kuhakikisha kwamba Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma zinafuatwa kikamilifu ili kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Umma. Maeneo yanayozingatiwa kwenye programu hiyo ni pamoja na: kuendelea kuboresha Mtandao wa malipo (IFMS) ili kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma kwa Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa; utoaji wa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo wa kibenki kwa watumishi wa Ofisi za Bunge, Sekretarieti za Mikoa, Idara ya Ushirika, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI na Ofisi za Hazina ndogo Mikoa yote. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya kuandaa hesabu kwa kutumia viwango vya uhasibu vya kimataifa ili kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za Umma; kuijengea uwezo Idara ya  Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma zinazingatiwa ipasavyo; na kujenga uwezo wa Serikali Kuu, Mikoa na Halmashauri katika eneo la uandaaji wa mipango na bajeti, ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa raslimali, uboreshaji wa mawasiliano na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa bajeti. 

86.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha utaratibu wa kupeleka fedha kwenye Halmashauri na kutoa taarifa mapema kuhusu matumizi ya fedha zilizopelekwa. Aidha, fedha zote zitakazovuka mwaka bila kutumika zitatolewa taarifa kwenye vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa umma.

87.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali itaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi kwenye Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote ili kuondoa watumishi wasiostahili kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali. Aidha, mamlaka za ajira na maafisa masuuli wanaelekezwa kusitisha malipo kwa watumishi walioacha au kuachishwa kazi, kustaafu, kufariki au likizo bila malipo ili kuzuia upotevu wa fedha za umma.

88.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutilia mkazo wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma katika Wizara, Taasisi, Wakala, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuthibitisha endapo fedha zinazopangwa kukusanywa zinapatikana na pia fedha zinazotumwa kutoka Hazina zinafika na kutekeleza shughuli zilizoidhinishwa. Serikali  itaboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa fedha za umma zinazokusanywa au kupelekwa kwenye Mikoa na Halmashauri nchini. 

Usimamizi wa Mashirika ya Umma

89.       Mheshimiwa Spika, katika kukabliana na changamoto za usimamizi wa Mashirika ya Umma, Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kufanya mapitio ya Sheria za Msajili wa Hazina ambazo ni “Treasury Registrar Ordinance” ya mwaka 1958 na “Treasury Registrar Powers and Functions” SURA 370 ya mwaka 2000 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 ili kuwa na Sheria moja.  Lengo la hatua hiyo ni kuimarisha ofisi kwa kuipa nguvu zaidi za kisheria kuweza kusimamia ipasavyo utendaji wa Mashirika ya Umma pamoja na Taasisi ili kuongeza tija.

Kukabiliana na Mfumuko wa Bei

90.       Mheshimiwa Spika, uchumi wetu unakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo mfumuko wa bei ambao kwa wastani umeshuka kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012. Kichocheo kikubwa cha mfumuko wa bei ni kupanda kwa bei za umeme, mafuta na vyakula hususan mchele na sukari. Kwa mfano kwa mwezi Aprili 2012, chakula kimechangia asilimia 24.7 wakati umeme na mafuta vimechangia kwa asilimia 24.9. Mfumuko wa bei ambao haujumuishi chakula na nishati bado uko kwenye tarakimu moja ambayo ni asilimia 8.8. Hivyo, jitihada za Serikali zitaelekezwa katika kukabiliana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizo.

91.       Mheshimiwa Spika, hatua za haraka ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa sukari na mchele kutoka nje na kuendelea kuimarisha Hifadhi ya Chakula ya Taifa. Aidha, Serikali itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Kilombero, Wami, Kagera na Malagarasi pamoja na miradi ya kilimo cha umwagiliaji. Hatua nyingine ni pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na masoko; kuimarisha mfumo wa masoko kwenye maeneo yanayozalisha chakula kwa wingi hususan mikoa ya nyanda za juu kusini na mipakani. Kwa upande wa nishati ya umeme, Serikali itaendeleza vyanzo mbadala vya umeme kama vile umeme wa gesi, nguvu za jua, upepo, miwa ili kupunguza matumizi ya mafuta kama chanzo cha nishati.

Kupanua fursa za Ajira

92.       Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ajira hasa kwa vijana, Serikali itaendelea kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki ya Kilimo na kuongeza mitaji kwa Benki za Rasilimali, Wanawake, Posta na Twiga Bancorp. Hatua nyingine zitakazochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo na mawasiliano. Aidha, sekta binafsi itahamasishwa kutumia fursa zinazotolewa na Benki na Maendeleo ya Afrika kupitia Dirisha la kuendeleza sekta binafsi. Kadhalika, Serikali itaajiri watumishi 71,756 katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na kada nyingine.
IV.       MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:

93.          Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imefanya maboresho katika mfumo wa kodi kwa nia ya kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya ndani.  Maboresho yaliyofanywa ni pamoja na marekebisho ya sheria za kodi, kanuni na taratibu za usimamiaji wa kodi. Aidha hatua hizi zimechangia katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. Hata hivyo kuna changamoto katika kuhuisha mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa bajeti hatua kwa hatua. Kwa
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.

94.          Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye mfumo wa kodi, napendekeza kufanya maboresho katika sheria mbalimbali za kodi kama ifuatavyo:-




a)    Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;

b)    Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;

c)     Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;

d)    Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;

e)    Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act),  SURA, 41;

f)     Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;

g)    Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;

h)    Misamaha ya Kodi ya magari kupitia sheria za kodi na   matangazo ya Serikali (GNs);

i)      Marekebisho mengine katika baadhi ya sheria za kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha; na




j)     Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.

k)    Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya  mwaka 2004;

A.   Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148

95.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo: -

              (i)      Kuanzisha kiwango kipya (VAT Rate) cha asilimia 10 cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa baadhi ya watu, taasisi na mashirika yanayopata unafuu wa kodi hiyo                                                          

(special relief). Kwa mantiki hiyo, wale waliokuwa hawalipi kodi hiyo kuanzia sasa watalipa asilimia 10. Hatua hii itazihusu Kampuni binafsi, watu binafsi na Kampuni zitakazopewa vyeti vya Kituo cha Uwekezaji Tanzania isipokuwa zile zenye vyeti hivyo kwa sasa. Aidha, itahusu pia Mashirika yasiyo ya Kiserikali isipokuwa yale yaliyopewa  msamaha wa kodi pale yanapotoa huduma ya chakula, dawa baridi na vifaa kama vile sabuni ambavyo vinatolewa msaada kwenye vituo mahsusi vya kulelea watoto yatima na shule;

             (ii)      Kurekebisha kifungu cha 19 cha Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kuongeza Mashine za Elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi (Electronic Fiscal Devices - “EFDs”) katika orodha ya vifaa vinavyopata msamaha wa kodi hiyo. Lengo ni kuwawezesha walipa kodi kupata vifaa hivi kwa gharama nafuu na kuhamasisha matumizi yake kwa kuwa ni muhimu katika kutoa stakabadhi za mauzo ya bidhaa na huduma;
            (iii)      Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya gesi iliyoshindiliwa na gesi ya mabomba (Compressed Natural Gas and Piped Natural Gas). Msamaha wa kodi unatolewa ili kuhamasisha matumizi ya gesi katika magari, kupikia, nyumbani, taasisi na viwandani. Aidha, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) litawajibika kuhakiki vifaa hivyo ili kuhakikisha kwamba vitatumika kujenga miundo mbinu ya gesi.

96.       Mheshimiwa Spika, Mitambo na vifaa vya kujenga miundombinu ya gesi asili vinavyoombewa msamaha wa kodi ni kama ifuatavyo:- 
  1. CNG vehicles conversion kits – vifaa vinavyoongezewa kwenye magari yaweze kutembea kwa kutumia nishati ya gesi asili;

  1. High pressure vessels (CNG and LPG cylinders) – mitungi maalumu ya kutunzia gesi asili iliyoshindiliwa na gesi ya LPG;
  2. Natural Gas Compression plants equipments – vifaa kwa ajili ya mitambo ya kushindilia gesi asili;

  1. Natural gas pipes (Transportation and Distribution pipes) – mabomba maalum ya kusafirishia na kusambazia gesi asili;

  1. CNG storage cascades – mitungi maalum ya pamoja ya kusafirishia na kuhifadhia gesi asili iliyoshindiliwa;

  1. CNG transportation trailers - magari na matela ya kusafirishia gesi asili iliyoshindiliwa;

  1. Natural gas metering equipments – mita za kupimia kiasi cha gesi asili;

  1. Pipeline fittings and valves – vifaa vya kuunganishia mabomba na kuruhusu/kuzuia gesi kupita;

  1. CNG Refueling/filling equipment – vifaa vya kujazia gesi asili kwenye magari;

  1. PNG/CNG accessories – vifaa vidogo vidogo vinavyotumika katika ujenzi wa mabomba ya gesi asili na katika mitambo ya kushindilia gesi asili;

  1. Gas Receiving Unit – vifaa vya kupokelea gesi ya mabomba;

  1. Condensate Stabilizer – vifaa vya mifumo ya kuimarisha uhifadhi wa condensate;

  1. Flare Gas System – vifaa kwa ajili ya mifumo ya kuunguza gesi kwa ajili ya usalama;

  1. Air & Nitrogen System – vifaa vya mifumo ya hewa na ya Nitrogen;

  1. Condensate Tanks and Loading Facility – matanki ya kuhifadhia condensate na vifaa vya kupakilia;

  1. System piping on piperack – mifumo ya kubeba mabomba ya gesi asili;
  2. Instrumentation – vifaa vya umeme na udhibiti kwenye mifumo ya gesi asili.

  1. Majiko yaliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya matumizi ya gesi pekee.

Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 22,565.1

B.         Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332

97.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -

  1. Kuweka kiwango cha chini cha mapato ghafi ya wafanyabiashara wadogo cha shilingi 3,000,000 kisichotozwa kodi na kurekebisha matabaka (bands) ya walipa kodi. Lengo la hatua hii ni kulinda mapato halisi ya Serikali na kuhakikisha kwamba wenye mapato ya chini ya kiwango cha kutozwa kodi cha shilingi 3,000,000 hawatozwi kodi chini ya mfumo wa kukadiria kodi Walipa kodi wadogo “Presumptive Scheme” kama ilivyo kwenye mapato yatokanayo na ajira. Hivi sasa Wafanyabiashara wenye kipato hicho wanatozwa Sh. 35,000.

 Viwango vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -
 Viwango vya sasa

Thamani ya Mauzo
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
(i)
Kwa mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/=
Shs. 35,000/=
1.1% ya mauzo
(ii)
Kwa mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/= na yasiyozidi Shs. 7,000,000/=
Shs. 95,000/=
Shs. 33,000/= + 1.3% ya mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/=
(iii)
Kwa mauzo yanayozidi Shs. 7,000,000/= na yasiyozidi Shs. 14,000,000/=
Shs. 291,000/=
Shs. 85,000/= + 2.5% ya mauzo yanayozidi  7,000,000/=
(iv)
Kwa mauzo yanayozidi Shs. 14,000,000/= na yasiyozidi Shs. 20,000,000/=
Shs. 520,000/=
Shs. 260,000/= + 3.3% ya mauzo yanayozidi  Shs. 14,000,000/=
 Viwango vinavyopendekezwa

Thamani ya Mauzo
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
(i)
Kwa mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/=
Asilimia sifuri (0%)
Asilimia sifuri (0%)
(ii)
Kwa mauzo yanayozidi Shs 3,000,000/= na yasiyozidi Shs 7,500,000/=
Shs. 100,000/=
2% ya mauzo yanayozidi
Shs 3,000,000/=
(iii)
Kwa mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/=  na yasiyozidi Shs 11,500,000/=
Shs. 212,000/=
Shs. 90,000/= plus 2.5% ya mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/=
(iv)
Kwa mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/=  na yasiyozidi Shs 16,000,000/=
Shs. 364,000/=
Shs. 190,000/= + 3.0% ya mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/=
(v)
Kwa mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/=  na yasiyozidi Shs 20,000,000/=
Shs. 575,000/=
Shs. 325,000/= + 3.5% ya mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/=






  1. Kutoza Kodi ya Zuio ya asilimia 10 kwenye mapato yatokanayo na riba inayotolewa na mabenki kwa wafanyabiashara ambao si wakaazi (non-residents). Lengo ni kuweka usawa kwa walipa kodi wote.

  1. Kufanya marekebisho ya kifungu cha 54 (2) cha sheria ya kodi ya mapato ili kufuta msamaha wa kodi ya mapato kwa makampuni yenye hisa zipatazo asilimia 25 au zaidi. Lengo la marekebisho haya ni kuleta usawa kwa walipa kodi wanapopata gawio.

  1. Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa raslimali  ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa hisa za kampuni za ndani unaofanywa na Kampuni mama ya nje ya nchi.

  1. Kuongeza kima cha chini cha kutozwa kodi (threshold) kwenye mapato ya ajira kutoka shilingi 135,000 hadi 170,000. Hatua hii itaongeza kipato kwa mfanyakazi.

  1. Kutoa msamaha wa Kodi ya Mapato kwa soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es salaam Stock Exchange). Lengo ni kulifanya soko hilo kukua.

  1. Kusamehe Kodi ya Mapato (kwa wenye leseni) yatokanayo na  michezo ya kubahatisha iliyokwishalipiwa kodi chini ya sheria ya kodi ya michezo ya kubahatisha, SURA 41. Lengo la hatua hii ni kuepusha wenye leseni za biashara ya michezo ya kubahatisha kulipa kodi mara mbili.

  1. Kusamehe Kodi ya Zuio kwenye riba ya mikopo inayotozwa na mabenki ya nje kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye sekta na shughuli muhimu katika mkakati wa kukuza uchumi (Strategic Investors).  Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wawekezaji hao wanapopata mikopo kutoka kwenye mabenki ya nje ya nchi na hivyo kuhamasisha uwekezaji hapa nchini.

Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 105,672.3

C.         Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147

98.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-

  1. Kufuta Ushuru wa bidhaa uliokuwa unatozwa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo. Hivi sasa mafuta hayo yanatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 40 kwa lita. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji katika viwanda hapa nchini. Aidha, hatua hii itaongeza uzalishaji na kuleta ushindani sawa kwa wenye viwanda katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa nchi nyingine hivi sasa hazitozi ushuru kwenye bidhaa hiyo.

  1. Mheshimiwa Spika,  kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya kudurufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini. Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia serikali mapato.



Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii utaanza rasmi tarehe 1 Januari, 2013.

  1. Kufuta msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo isipokuwa kwa miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mkataba, mashirika ya dini, Balozi, Ofisi za Balozi, Wanabalozi na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic Missions). Aidha haitahusu Kampuni za Madini zenye mikataba yenye kutoa misamaha.

  1. Ili kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyotengeneza maji ya matunda (juisi) dhidi ya ushindani usio haki wa bidhaa hiyo kutoka nje, maji ya matunda kutoka nje yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 83 kwa lita ambapo yanayozalishwa hapa nchini yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 8 tu kwa lita.;

  1. Kurejea msamaha wa ushuru wa mafuta ya petroli (fuel levy) uliotolewa mwaka 2011/12 kwenye mafuta yanayotumika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili usomeke kama Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwenye mafuta ya Petroli.

  1. Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe, vinywaji baridi, sigara, na mvinyo kama ifuatavyo: -

a.     Vinywaji baridi kutoka shilingi 69 kwa lita hadi shilingi 83 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya shilingi 14;

b.     Mvinyo uliotengenezwa kwa Zabibu inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 145 kwa lita, ikiwa ni punguzo la shilingi 275;
c.     Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 1,345 kwa lita hadi shilingi 1,614  kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 269;

d.     Vinywaji vikali, kutoka shilingi 1,993 kwa lita hadi shilingi 2,392 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 399.

e.     Bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 248 kwa lita hadi shilingi 310 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 62;

f.      Bia nyingine zote, kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 525 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 105 sawa na shilingi 52.5 kwa chupa yenye ujazo wa nusu lita;


Marekebisho ya viwango vya Ushuru wa bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: -

a)            Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 6,820  hadi shilingi 8,210 kwa sigara elfu moja. Hii ni sawa na nyongeza ya shilingi 1,390 kwa sigara elfu moja au shilingi 1.4 kwa sigara moja;

b)            Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 16,114 hadi shilingi 19,410 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 3,296 au shilingi 3.3 kwa sigara moja;



c)             Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 29,264  hadi shilingi 35,117  kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 5,853 sawa na shilingi 5.8 kwa sigara moja;

d)            Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi 14,780  hadi shilingi 17,736 kwa kilo, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 2,956 kwa kilo; na,

e)            Ushuru wa “Cigar” unabaki kuwa asilimia 30.

  1. Kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye Gesi asilia inayotumika viwandani  kwa kiwango cha Shilingi 0.35 kwa kila futi ya ujazo (Shs 0.35 per cubic feet);

  1. Kuongeza Ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 12. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa huduma hii katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wakati huu ambapo tupo kwenye soko la pamoja.

Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 144,054.9

D.         Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, Sura 196;

99.       Mheshimiwa Spika,  napendekeza kuongeza kiwango cha Ushuru wa mauzo nje (export levy) kwenye bidhaa za ngozi ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka asilimia 40 za sasa au Shilingi 400 kwa kilo moja hadi asilimia 90 au Shilingi 900 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa.  Lengo la hatua hii ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hapa nchini na kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi. Aidha hatua hii itachangia katika kukuza ajira viwandani na kuongeza mapato ya Serikali.

 Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 26,431.8



E.         Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act),  SURA, 41;

100.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA 41; kama ifuatavyo:-
              i.        Kuongeza tozo la Gaming Tax kwa casino kutoka asilimia 13 ya mapato ghafi ya mchezo wa kubahatisha (Gross Gaming Revenue) hadi asilimia 15;

             ii.        Kutoza tozo kwenye michezo ya Utabiri wa matokeo ya michezo (Sports Betting) kwa asilimia 6 ya “total stakes”;

            iii.        Kutoza tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 43 kwenye michezo ya “SMS Lotteries”;

            iv.        Kutoza tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 15 kwa michezo ya Internet Casino.


             v.        Kuweka kipengele katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya kubahatisha kinachotamka kwamba “gaming tax shall be conclusive tax”.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 6,360.

F.         Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;

101. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124 kwa kuanzisha utaratibu wa kumiliki usajili wa namba za magari zenye utambulisho wa taarifa za mtu binafsi kwenye gari lake kwa ada ya shilingi 5,000,000 kwa miaka mitatu.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 50


G.         Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;

102.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365 kwa kuongeza tozo ya huduma za viwanja vya ndege (Airport Service Charges) kutoka kiwango cha sasa cha Dola za Kimarekani 30 hadi Dola 40 kwa safari za nje na kutoka Shilingi za Tanzania 5,000 hadi Shilingi 10,000 kwa safari za ndani.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 11,597.7

H.         Misamaha ya kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs)

103.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria husika za kodi na matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa kodi kwenye magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka nane (8) kwa magari hayo badala ya miaka 10. Aidha, magari yenye umri wa zaidi ya miaka nane (8) yatatozwa Ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu na kulinda mazingira.

I.          Marekebisho mengine katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha

104.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.

105.       Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, SURA 231 ili kwanza, kuweka kinga dhidi ya mali zinazomilikiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ikiwemo nyumba, akiba, fedha na akaunti za benki dhidi ya mashauri ya kisheria, maamuzi ya kimahakama na utaifishaji. Pili, kuipa hadhi ya mdai benki hii kama ilivyo kwa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuiwezesha kupewa upendeleo endapo yatatokea matatizo yoyote katika soko la fedha. Tatu, kumpa mamlaka Waziri wa Fedha kutekeleza maamuzi ya Baraza la uongozi (Governing Board) la EADB kwa kurekebisha Jedwali la Sheria hii kupitia Tangazo la Serikali na baadaye kuwasilisha taarifa Bungeni. Nne, kutoa tafsiri ya mali za benki ili kutoa ufafanuzi kwamba mali za benki ni pamoja na nyumba za benki, akiba za fedha zilizokasimiwa kwa EADB kwa ajili ya utendaji wake.

J.         Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea

106.     Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi. 

K.         Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004

107.     Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya Kikao cha maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) mnamo tarehe 18 Mei 2012 jijini Kampala, Uganda. Kikao hicho kilipendekeza marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC-Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha wa 2012/13.  Mapendekezo hayo yanalenga katika kuboresha Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Afya, Nishati, Mifugo, Mawasiliano na Habari.

108.     Mheshimiwa Spika, maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni: -

      i.        Kutoza ushuru wa asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 35 kwenye ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.90.20 na HS Code 1001.90.90 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uingizaji wa bidhaa hii nchini kwa vile uzalishaji wa ndani bado ni wa chini kuweza kutosheleza mahitaji.

     ii.        Kuongeza Ushuru wa Forodha kwenye galvanized wire kutoka asilimia sifuri (0%) hadi asilimia 10 inayotambuliwa katika HS Code 7217.20.00. Hatua hii inalenga katika kuwianisha viwango vya utozaji wa Ushuru wa Forodha kwa vile bidhaa hii inatengenezwa kutokana na hot rolled steel wire rods zinazotambuliwa katika HS Code 7213.20.00 ambayo inatozwa ushuru wa asilimia 10.

    iii.        Kutenganishwa kwa bidhaa zinazotambulika katika HS Code 2106.90.91 ili kutenganisha virutubisho vya chakula na madini (food supplements and mineral premix) vinavyotumika katika kutengeneza chakula cha watoto wachanga na kuzitoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika kuwezesha watoto wachanga na wagonjwa kuweza kupata vyakula vyenye virutubisho kwa bei nafuu na kuimarisha afya zao.

    iv.        Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri kwenye ving’amuzi (set top boxes) vinavyotambuliwa katika HS Code 8528.71.00 ili kuwezesha mabadiliko ya kutoka katika teknolojia ya analogi na kwenda katika teknolojia ya digitali. Hatua hii inatekeleza makubaliano ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba ifikapo Desemba 2015 ziwe zimetoka kwenye mfumo wa utangazaji wa analogi kwenda digitali.

     v.        Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye umeme (HS Code 2716.00.00) kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama ya umeme unaonunuliwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji katika nchi hizo.

    vi.        Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye glasi za ndani (inner glass) za chupa za chai (thermos) zinozotambuliwa katika HS Code 7020.00.90 kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri ili kutoa unafuu na kuchochea ukuaji wa viwanda vya kuunganisha chupa za chai katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa bidhaa hiyo haipatikani katika Jumuiya.

   vii.        Kutenganisha programu (software) inayotambulika katika HS Code 8523.80.00 ili kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Lengo ni kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano na hivyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

  viii.        Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwenye malighafi ya kutengeneza sabuni (Palm Sterini, RBD) inayotambuliwa katika HS Code 1511.90.40 kwa kipindi cha mwaka moja. Hatua hii inalenga katika kuvipa unafuu viwanda vidogo vya kutengeneza sabuni hapa nchini na kuviwezesha kumudu ushindani katika bidhaa hiyo inapoingizwa kutoka nje.


    ix.        Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa malighafi ya kutengeneza sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuimarisha uzalishaji na kukuza viwanda vidogo vya sabuni nchini.

     x.        Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye bidhaa inayojulikana kama cathodes inayotambuliwa katika HS Code 7403.11.00 kutoka asilimia 10 hadi sifuri (0%). Hivi sasa bidhaa hii inatozwa ushuru wa asilimia 10 ambapo shaba iliyotengenezwa kwa ukamilifu (refined alloys/refined copper) hutozwa ushuru wa asilimia (0%), ambapo ni kinyume na matakwa ya sheria ya ushuru wa forodha ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa malighafi inayotumika kuzalisha bidhaa hii ili iendane na kanuni/taratibu za kutoza ushuru zinazozingatia viwango vya usindikaji.

    xi.        Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 35 kwenye saruji inayotambuliwa katika HS Code 2523.90.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

   xii.        Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa wazalishaji wanaotumia mafuta ya kutengeneza vilainishi (castor oil and its fraction) inayotambuliwa katika HS Code 1515.30.00 Hatua hii imezingatia kwamba bidhaa hii ni mali ghafi inayotumika katika kutengeneza vilainishi;

  xiii.        Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za barabara vijulikanavyo kama road guard rails kwa kutenganisha HS Code 7308.90.90. Lengo ni kutoa unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bidhaa hii haizalishwi kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki;



109.     Mheshimiwa Spika,  Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-

      i.        Kufanya marekebisho katika Kifungu 30(b) cha Sehemu B ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini.  Msamaha huu hautahusisha vipuri vya magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na uchimbaji wa madini.

     ii.        Kufanya marekebisho katika aya ya 22 (a) ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza “refrigerated trailers” katika bidhaa zinazopata msamaha wa Ushuru wa Forodha. Hatua hii inalenga katika kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari ya trela yenye majokofu ili kuimarisha biashara ya usambazaji bidhaa kama vile nyama, maziwa n.k.

    iii.        Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi zinazotumika katika kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa (medical diagnostic kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri (0%) vinapoagizwa kutoka nje. Aidha, lengo pia ni kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    iv.        Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano, B kwenye aya ya 15 ili kuongeza vifaa vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali na kuvipa msamaha wa ushuru wa forodha vinapoagizwa nje na wafugaji wa nyuki. Lengo ni kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa nyuki.

     v.        Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha mwaka mmoja.


    vi.        Kufanya marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa wazalishaji wa vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa lishe ya watoto wenye utapia mlo na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Hatua hii inalenga katika kuwawezesha kupata vyakula hivyo kwa gharama nafuu na kuboresha afya zao.

110.     Mheshimiwa Spika, Marekebisho mengine ninayotarajia kufanya kwenye Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -

      i.        Kufuta msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa magari yenye ujazo wa cc 3000. Hatua hii haitahusu miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mikataba, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic missions).

     ii.        Kupunguza msamaha wa kodi uliokuwa unatolewa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “deemed capital goods” kutoka asilimia 100 hadi asilimia 90.   Kwa mantiki hiyo, mwekezaji atatakiwa kulipa asilimia 10 ya kodi zote zinazotozwa kwenye bidhaa husika.

Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 12,805

Mheshimiwa Spika, hatua zote za mapato kwa ujumla zimezingatia azma ya Serikali ya kukuza uchumi na kuongeza mapato ili hatimaye kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani. Aidha, ili kutekeleza azma hiyo, hatua za mapato zinalenga katika kupunguza misamaha ya kodi hatua kwa hatua ili kufikia kiwango cha asilimia 1 ya Pato la Taifa kama ilivyo katika nchi nyingine Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

L.         Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi



111.     Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2012, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo. 

V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2012/13

112.     Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, Serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni 15,119.6. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 8,714.8 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.

113.     Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutusaidia mwakani kwa kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 3,156.7. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 842.5 ni misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,314.2 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikijumuisha Basket Funds na fedha za Millenium Challenge Account (MCA - T).

114.     Mheshimiwa Spika, Serikali inategemea kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,886.1 kutoka vyanzo vya ndani na nje kuziba pengo la mapato. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva, shilingi bilioni 483.9 ambayo ni asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,254.1 ni mikopo yenye masharti ya kibiashara.

115.     Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 15,119.6 katika mwaka 2012/13 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Jumla ya shilingi bilioni 10,591.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha shilingi bilioni 3,781.1 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Taasisi na Wakala za Serikali na shilingi bilioni 2,745.1 kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 4,527.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,213.6 kitagharamiwa kwa fedha za ndani na shilingi bilioni 2,314.2 kitagharamiwa kwa fedha za nje (misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha miradi ya MCA (T) na basket fund).

116.     Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2012/13 inakuwa kama ifuatavyo:-


Mapato
Shilingi Milioni
A.
Mapato ya Ndani

8,714,671

(i)   Mapato ya Kodi (TRA)
8,070,088


(ii)  Mapato yasiyo ya Kodi
644,583

B.
Mapato ya Halmashauri

362,206
C.
Mikopo na Misaada ya Kibajeti

842,487
D.
Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha MCA (T)

2,314,231
E.
Mikopo ya Ndani

1,631,957
F.
Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara

1,254,092

JUMLA YA MAPATO YOTE

15,119,644

Matumizi
G.
Matumizi ya Kawaida

10,591,805

(i)    Deni la Taifa
2,745,056


(ii)   Mishahara
3,781,100


(iii)  Matumizi Mengineyo
4,065,649


      Wizara               3,311,399



      Mikoa                     49,701



      Halmashauri         704,549


H.
Matumizi ya Maendeleo

4,527,839

(i)  Fedha za Ndani
2,213,608


(ii)  Fedha za Nje
2,314,231


JUMLA YA MATUMIZI YOTE

15,119,644







117.     Mheshimiwa Spika, mambo yaliyozingatiwa wakati wa mgao wa fedha kwa bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na yafuatayo:-


i.              Kuweka mafungu yote katika kiwango cha mgao wa fedha kinacholingana na matarajio ya matumizi ya mafungu husika kwa mwaka 2011/12;


ii.             Kuyatengea fedha matumizi yasiyoepukika kama vile posho za kisheria, “ration allowance”, nk.


iii.            Maeneo mapya ya utawala;


iv.            Fedha zinazotolewa kwa wizara zenye utaratibu wa kubakiza (retention);


v.             Maeneo ya vipaumbele (strategic na non-strategic).


118.     Mheshimiwa Spika, bajeti ninayoiwasilisha ina uwiano wa asilimia 70 kwa matumizi ya kawaida na asilimia 30 kwa  matumizi ya maendeleo.  Viwango hivyo vya uwiano vimezingatia ukweli kwamba makisio ya matumizi ya maendeleo kwa fedha za ndani ya Shilingi 1,871.5 bilioni na makisio ya matumizi ya maendeleo kwa fedha za nje ya Shilingi 3,054.1 bilioni yenye jumla ya Shilingi 4,925.6 kwa mwaka 2011/12 hayatafikiwa.  Hivyo, inatarajiwa kwamba hali halisi ya matumizi ya maendeleo itakuwa Shilingi 2,983 bilioni ambayo ni karibu ya asilimia 22. Kwa kipindi kilichoishia Aprili, 2012 matumizi ya maendeleo kwa fedha za ndani yalifikia 1,201.6 bilioni na matumizi ya maendeleo kwa fedha za nje ni shilingi 1,450.4 bilioni. Sababu za kutofikiwa kwa malengo hayo ya matumizi nimezieleza hapo awali ikiwa ni pamoja na kutopatikana kwa fedha za mikopo ya kibiashara na kuchelewa kwa fedha za misaada na mikopo ya  miradi ya maendeleo kutoka kwa wahisani.  Aidha, uwiano huo umezingatia maeneo niliyoyataja hapo juu ambayo ni matumizi muhimu.

VI.       HITIMISHO

119.     Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia bajeti hii imejipanga kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ambao unaelekeza uwekezaji wa rasilimali za Taifa kwenye maeneo machache ya kipaumbele kwa lengo la kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini. Serikali itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Aidha, kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika kutumia fursa zinazojitokeza kwa kutoa huduma na kuzalisha mali ili kujiongezea kipato.


120.     Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti ya Mwaka 2012/13 kunahitaji nidhamu ya hali ya juu kwa kila Wizara, Idara, Mikoa, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma. Matumizi yasiyokuwa na tija na ambayo si muhimu ni vyema yakaepukwa. Sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa kuchangia katika uchumi. Hivyo, ni muhimu kila Wizara, Idara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa fursa kwa sekta binafsi ili waweze kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa letu.

121.     Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka huu unafanyika miezi michache kabla ya zoezi muhimu la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti 2012. Kauli mbiu ya sensa ya mwaka huu ni ‘‘Sensa kwa Maendeleo Jiandae Kuhesabiwa’’. Napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine katika ngazi zote kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hili ambalo matokeo yake yatawezesha kupata takwimu muhimu zitakazowezesha Serikali kupanga mipango kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kwa usahihi.

122.     Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wote wa Jimbo la Kalenga kwa kunichagua kuwa Mbunge wao na kwa ushirikiano wanaonipatia. Napenda kuwaahidi kuwa nitaendelea kushirikiana nanyi kuliletea maendeleo Jimbo letu la Kalenga. Mwisho namshukuru mke wangu mpendwa pamoja na familia kwa kuwa msaada kwangu katika kutekeleza majukumu haya mapya.

123.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


No comments:

Post a Comment