Saturday, June 23, 2012

MAKALA YA SHOMARI KAPOMBE SEHEMU YA PILI: AWATAJA WALIOCHANGIA MAFANIKIO YAKE NA YALIYOMKUTA AKIWA ANGANI KUELEKEA CAMEROON.

***MO BLOG kama ilivyokuahidi sasa tunakuletea sehemu ya pili ya makala inayomchambua Mchezaji Bora wa Chama cha waandishi wa habari tanzania (TASWA) Shomari Kapombe ambapo tunazungumzia ‘alikotokea kisoka, maisha ya kuokota mipira uwanjani, watu waliochangia mafanikio yake, alitua vipi Msimbazi na sifa za ziada na asichokisahau maishani kwake***.
AMETOKEA WAPI KISOKA.
Kapombe anasema alianza kupenda soka tangu akiwa na miaka mitano, wakati huo akicheza chandimu mtaani kwao Mafiga, Morogoro.
Anasema timu yake ya kwanza ni Santos FC, iliyokuwa ikishiriki michuano mbalimbali, akipata nafasi ya kujifunza mengi ya soka.
Kati ya michuano aliyowahi kucheza akiwa na Santos FC ni ‘Serve Access Game’ iliyokuwa ikiandaliwa na taasisi ya kuibua vipaji ya  Morogoro Youth Academy .
KUOKOTA MIPIRA UWANJANI
 Mbali ya kucheza Santos FC pia Kapombe alikuwa kwenye timu iliyokuwa ikiundwa na vijana waokota mipira kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro iliyojulikana kwa jina la ‘Jamhuri Ball Boys FC’.
 “Nilipitia timu nyingi katika utoto wangu, Mafiga FC, Santos, Jamhuri Ball Boys, hadi nikaonwa na kituo cha Moro Youth Academy,” anasema Kapombe.
Anasema, kote alikopitia kisoka kwenye utoto wake, ndoto yake ilikuwa ni kufika mbali kisoka, hivyo kutwaa tuzo ya Taswa, ni mwanzo kwake.
“Nikiwa Ball Boys pale uwanja wa Jamhuri, nilikuwa na shauku kubwa ya kucheza timu kubwa kama Mtibwa Sugar, Simba, Yanga na nyinginezo nilizokuwa naziona Jamhuri.
“Nilijipa moyo, nikiongeza juhudi zangu katika mazoezi kutimiza ndoto hizo, kweli zimeanza kutimia,” anasema Kapombe.
Akiwa na umri wa miaka 14, wakati huo akiichezea Ball Boys, alipewa unahodha katika michuano ya WINOME Cup na Serve Access Games.
Baada ya kung’ara, ndipo akatwaliwa na kituo Moro Youth, hivyo kupata nafasi ya kujifunza mengi zaidi.


ALITUA VIPI SIMBA?
Anasema Simba walimwona katika mechi ya kimataifa dhidi ya Cameroon kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .
Baada ya filimbi ya mwisho, alifuatwa na viongozi wa Simba wakimtaka ajiunge nayo, naye hakusita kwani ni kitu ambacho hakuwa amekitarajia katika umri wa miaka 17.
Anasema baada ya kutua Simba, mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya timu kutoka Uganda kwenye Simba Day, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Wakiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Moses Basena, akatangaza nyota 18 huku akimpa jezi namba 15 ya kikosi cha kwanza.
Mbali ya kupewa jezi, Basena alimsihi kucheza kwa kujiamini na mechi kubwa kwake ilikuwa mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga, akiingia kutokea benchi.
Kapombe anasema, anashukuru Mungu kumjalia uwezo kisoka kwani msimu wake wa kwanza akiwa Simba, ameweza kupangwa kikosi cha kwanza katika mechi zote.
HISTORIA KWA UFUPI
Kapombe ni mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto watatu wa Mzee Salum Kapombe wa mjini Morogoro, aliyezaliwa Januari 28, 1992.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Mwele, kuanzia 2000 hadi 2006 na baadaye elimu ya sekondari ya Lupanga.
Hiyo ni shule iliyo jirani na Chuo cha Ualimu Kigurunyembe, kuanzia 2007 hadi 2010.
 SIFA ZA ZIADA
 Amejaliwa uwezo wa kutumia miguu yote miwili, pia amekuwa akicheza namba zaidi ya moja ikiwemo kudaka.
Kapombe amekuwa akivutiwa na Haruna Moshi ‘Boban,’ akisema ndiye amekuwa akiiga uchezaji wake kwa hapa nchini.
Kimataifa, amekuwa akivutiwa na Tom Cleverley wa timu ya Manchester Utd ya England .
 SHUKRANI
Anasema hawezi kuwasahau makocha, wazazi wake na wengine wengi wakiwemo Catherine Ntevi, Godfrey Ngatimwa na Dennis Anthony kwani wamekuwa msaada mkubwa akiwa jijini Dar es Salaam .
Aidha, anawashukuru makocha Belin, Allan Thigo na Rajabu Kindagule wa Moro Youth, John Tamba wa Polisi Morogoro, ‘Julio’, Moses Basena wa Simba Jan Poulsen aliyemwita mara ya kwanza Stars.
ASICHOKISAHAU
Kapombe anasema katika maisha yake hatosahu walipokuwa safarini kuelekea mjini Younde , Cameroon mwanzoni mwa mwaka huu ambapo wakiwa angani, walikumbana na hali mbaya ya hewa hadi ndege kuanza kuyumba, hali ile ilimuweka kwenye wakati mgumu.
DONDOO MUHIMU;
 JINA KAMILI: Shomari Salum Kapombe.
KUZALIWA: Januari 28, 1992.
MAHALI: Morogoro.
TIMU YA MTAANI: Santos Fc, Mafiga Kids
UTAIFA: Tanzania
ELIMU: Kidato cha nne
Mwandishi wa makala: 0719076376/chalefamily@yahoo.com



No comments:

Post a Comment