Mmarekani Chris Wilder anatarajia kuipa Tanzania zawadi ya kusheherekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika atakapokimbia kilometa 1 kwa kila mwaka wa uhuru wa Tanganyika/Tanzania.
Hii ina maana atakimbia kilometa 50 kusheherekea uhuru wa Tanganyika uliopatikana mwaka 1961.
Chris wilder ni Physician Assistant kutoka Annapolis, Maryland nchini Marekani na yuko mjini Moshi kukimbia mbio za 22 za Mt. Kilimanjaro Marathon tarehe 24 Juni mwaka huu.
Mbio hizi zitaanzia Moshi Klabu mpaka Rau madukani na kurudi mara tatu.
Kutakuwa na mbio za kilometa 42, Kilometa 21, Kilometa 10 na Kilometa 5.
Mbio za Mount Kilimanjaro Marathon zilianzishwa na mama Marie Frances anayetoka katika mji wa Bethesda Marekani mwaka 1991 katika mji wa Moshi baada ya kuombwa na balozi wa zamani wa Tanzania nchini Misri kuja kuanzisha mbio za Marathon ili kuitangaza Tanzania.
Kila mwaka Jumapili ya mwisho ya mwezi wa sita mbio za Mount Kilimanjaro marathon zimekuwa zinafanyika.
Kwa kutambua mchango wake katika kuutangaza mji wa Moshi tangu mwaka 1991, Manispaa ya Moshi ilimzawadia Marie Frances barabara ya zamani ya Bustani Ale na kuiita Marie Frances Boulevard.
Aidha Frances alipewa funguo za Manispaa na kufanywa mkazi wa kudumu wa Manispaa ya Moshi katika shereke zilizofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Moshi mwaka 2009.
Mbio za mwaka huu za Mt. Kilimanjaro marathon zitapambwa na mcheza sinema maarufu wa Marekani Deidre Lorenz anayetarajiwa mjini Moshi tarehe 21 mwezi huu, kushiriki kwenye mbio hizo maarufu.
Miss Lorenz ameshiriki kwenye sinema nyingi kama vile Santorini Blue, Perfect Strangers, The Great Fight na nyingine nyingi.
Chris Wilde ni mkimbiaji wa mbio za marathon za Ultra Marathon na mwaka jana alikimbia kilometa 100.
Kwa kukimbia kwake kilometa 50 na kuizawadia Tanzania, Wilde ataweka historia ya mtu aliyekuja kupanda mlima Kilimanjaro na kukimbia kilometa 50 kama zawadi ya nchi hii tukufu.
No comments:
Post a Comment