Monday, June 25, 2012

WAKULIMA WA ALIZETI MKOANI SINGIDA WAPIGWA MARUFUKU KUUZA KWA WANUNUZI BINAFSI.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone, akitoa amri halali ya kupiga marufuku wanunuzi binafsi kununua Alizeti kwa wakulima na badala yake kazi hiyo itafanywa na vyama vya msingi vya ushirika.
Baadhi ya waandishi wa habari (walioketi mbele) na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika mkoani Singida wakimsikiliza mkuu wa mkoa Dk.Parseko Vicent Kone (hayupo pichani) akitoa amri halali ya kupiga marufuku wanunnuzi binafsi kununua alizeti.Kazi hiyo ya ununuzi wa zao la Alizeti,sasa itafanywa na vyama vya msingi vya ushirika pekee.Lengo ni mkulima kunufaika na kilimo cha zao hilo.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone, amepiga marufuku wanunuzi binafsi kununua zao la alizeti kutoka kwa wakulima.
Amri hiyo halali,imeanza kutekelezwa kuanzia  juzi msimu huu wa mwaka 2011/2012 na kuendelea.
Dk.Kone ametoa amri hiyo halali,juzi wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi yake mjini hapa.
Alisema lengo la amri hiyo, ni kutoa fursa kwa vyama vya ushirika kuwa wanunuzi pekee wa zao hilo la alizeti ambapo msimu uliopita,liliingizia mkoa pato la zaidi ya shilingi bilioni sita.
Dk.Kone alisema serikali mkoani Singida,imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa wanunuzi binafsi wamekuwa wakiwanyonya wakulima kwa kununua alizeti kwa bei ndogo sana.
“Pia mkoa umekuwa ukikosa takwimu sahihi za uzalishaji wa alizeti na mbaya zaidi, wanunuzi wamekuwa wakitorosha zao hili kwa njia ya panya, hivyo mkoa kukosa pato litokananlo na alizeti”,alisema Dk.Kone.
Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumiwa na vyama vya msingi vya ushirika, ndio mfumo pekee ambao unaweza kumsaidia mkulima mdogo kupata pato linalolingana na jasho lake.
 ”Lengo kuu la muda mrefu la maendeleo ya Tanzania kwa kizazi kijacho kama ilivyoainishwa kwenye dira ya maendeleo ya Tanzania 2025, ni kupatikana kwa maendeleo endelevu ya binadamu.Kwa hiyo, ushirika ni mojawapo ya nyenzo kukufanikisha dira hiyo”,alisema.
Mkuu huyo wa mkoa, alitoa amri hiyo,alisema “kuanzia juni 21 mwaka huu, na kuendelea vyama vya ushirika vya msingi, ndivyo pekee vitaruhusiwa kununua zoa la alizeti toka kwa wakulima.Wanunuzi binafsi, watanunua alizeti kwenye maghala kwa maelekezo ya chama kikuu cha ushirika, SIFACU na kwa bei watakayokubaliana”.
Mkutano huo wa mkuu wa mkoa wa waandishi wa habari, ulihudhuriwa pia na mwenyekiti wa SIFACU Omari Nyuda na viongozi wa vyama vya ushirika 551.



No comments:

Post a Comment