Wednesday, June 20, 2012

“WAMILIKI WA JAMII FORUMS NI WATANZANIA WANAOITUMIA”-MAXENCE MELO (MAHOJIANO MAALUM) Read more:


Tukiamua kubishana,tunaweza kufanya hivyo. Lakini endapo mwisho wa ubishi huo tutaamua kukubaliana,basi sina shaka kwamba sote tutakubaliana kwamba; miongoni mwa mitandao inayotembelewa na yenye ushawishi mkubwa na wa aina yake miongoni mwa watanzania wengi,mtandao wa Jamii Forums au kwa kifupi JF hauwezi kukosa katika orodha hiyo.

Lakini tofauti na mitandao mingine ambayo kimsingi imekuwa ikiendeshwa na mtu au watu wachache tu, JF ni mtandao unaondeshwa na watu wengi.Wengi wakiwa watanzania wenyewe. Pengine hiki ndicho kinachoufanya mtandao wa Jamii Forums kuwa na “upekee” kama nilivyogusia hapo juu.

Uendeshwaji huu wa jumla unafanyika kwa uhuru wa kila mtu kujiunga na kuanzisha mjadala,kuchangia au kuupanua zaidi. Kimsingi,hivyo ndivyo mtandao wa Jamii Forumsunavyochanja mbuga hivi leo. Wewe na mimi sote tunaweza kujiunga na kuendeleza mijadala. Ndani ya Jamii Forums kuna watu wa kila aina.Kuna watanzania.Kuna viongozi/wanasiasa,wanataaluma mbalimbali na pia kuna wenzangu na mie,watu wa kawaida wenye mapenzi na tekinolojia,habari,maarifa na wenye kutafuta mahali pa kutolea maoni yao huku wakiwa na imani kubwa kwamba kuna mtu atasoma ,kusikia na kuyafanyia kazi.
Ulianzaje? Nini malengo yake?Ni kweli kwamba mtandao huu unamilikiwa na chama fulani cha kisiasa? Mtandao huu una malengo gani?
Ili kupata majibu kwa maswali lukuki niliyokuwa nayo(na bila shaka uliyonayo wewe msomaji) nilimtafuta Maxence Melo Mubyazi(pichani), ambaye ni mwanzilishi-mwenza waJamii Forums na mtu ambaye mpaka hivi leo anabakia kuwa mhimili wa Jamii Forums ili kupata baadhi ya majibu kwa maswali yangu. Haya hapa ni mahojiano yangu naye;

BC: Kawaida mtu anapoanzisha kitu cha mtandaoni huwa ana malengo fulani ingawa inaweza ikatokea kwamba hapo baadae malengo yakabadilika au kujinyambulisha kidogo ili kwenda na wakati na hali halisi. Kwa upande wenu, mlikuwa na malengo gani kimsingi mlipoanzisha Jamii Forums? Je, bado malengo ni yale yale au yamebadilika?

MM: Malengo yetu tangu mwanzo ni yale yale na hayajabadilika na wala hatudhanii yatabadilika karibuni; kutoa uhuru wa kujieleza kwa njia mbadala. Ni wazi kuwa hili linaendelea japo linakuwa ndani ya sheria (http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/18042-jamiiforums-rules.html ) tulizojiwekea tangu mapema 2006.

BC: Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Jamii Forums kwamba nyie Moderators wakati mwingine mmekuwa mkionyesha utashi binafsi. Mmewahi kulalamikiwa kwamba huwa mnatoa thread fulani kwa sababu zenu binafsi. Unasemaje kuhusu tuhuma kama hizi na labda unaweza kutusaidia kuelewa ni kitu au sababu gani zinaweza kusababisha “thread” fulani kuondolewa?

MM: Kama nilivyotangulia kusema tangu mwanzo; moderators wa JF wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria za uendeshaji JF; ufafanuzi juu ya thread (topic) gani huondolewa na kwa vigezo gani upo wazi http://www.jamiiforums.com/habari-na-hoja-mchanganyiko/69153-topic-gani-hufungwa-au-kufutwa-kabisa-jf.html na tuliutoa baada ya malalamiko ya wengi. Kila kitu kiko wazi, wengi wa wanaolalamika huwa hawapendi kuumiza vichwa, wale wanaowasiliana nasi huwa tunawapa ufafanuzi. Kuna kipindi tuliweka ‘automated notifications’ pindi thread inapohamishwa au kufutwa, tulichoambulia ilikuwa ni kazi bure, watu hawasomi hizo notifications!

Kila binadamu ana mapungufu, lakini hatuwezi kusema kuwa tutafanya kazi kwa hisia tu. Kuna moderation tools, moderator akifanya makosa yanaonekana kwa wote kuwa aliyefanya kosa ni moderator gani hivyo wote tunawajibika kurekebisha kosa la mmoja. Nyakati nyingine huwa tunalazimika kuomba radhi kutokana na makosa yanayoweza kutokea tokana na utendaji wa mmoja wetu.

Tuseme ukweli, uhuru bila mipaka wakati mwingine ni fujo. Huwezi kuruhusu mijadala ambayo inachochea umwagikaji damu, inachochea vurugu ama inajenga utengano miongoni mwa watanzania bila kufikiria athari za mbeleni kwa taifa letu.

Tunaijua hulka ya mwanadamu; wakati mwingine akishaweka kitu flani kichwani mwake basi kukibadili inakuwa kazi kubwa. Mtu anayeanzisha mjadala wa uchokonozi wa kidini ama kikabila ama kuanzisha mjadala ambao hana ushahidi ili mradi anataka kuchangamsha jamvi tu anakuwa anajua wazi anachofanya si kizuri lakini anafanya hivyo akiwa kajiandaa kuwashambulia viranja wa jukwaa (moderators).

No comments:

Post a Comment