Friday, June 22, 2012

YONDANI AWAKATA 'STIMU' MASHABIKI YANGA


Waandishi Wetu
MAMIA ya wapenzi na mashabiki wa Yanga waliofika Makao Makuu ya klabu hiyo jana asubuhi na jioni  walipigwa na butwaa baada ya ndoto zao za kutaka kumwona beki mpya wa timu hiyo, Kelvin Yondani akiwa katika uzi ya njano kugonga mwamba.

Kelvin aliyevuta hisia za mashabiki wa soka baada ya kila upande, Simba na Yanga kudai wana haki naye, kabla ya mchezaji huyo kuvunja ukimya na kusema hayuko tayari kuichezea Simba msimu ujao. Inadaiwa Yondani alivuta Sh30mil kusajili Yanga.

Hali hiyo iliwafanya mashabiki hao, wake kwa waume waliokuwa wamefika klabuni hapo kwa lengo la kumpokea mchezaji huyo kutawaliwa na maswali mengi akilini mwao huku wakiutaka uongozi wa timu hiyo kuweka wazi siku ambayo mchezaji huyo atajiunga na wenzake kujiandaa na Michuano ya Kagame.

Kikosi cha Yanga hivi sasa kipo katika maandalizi makali ya michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Julai 14 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

"Viongozi wetu wametuchanganya kwani umati huu unavyouona hapa ulikuja kwa ajili ya kumpokea Yondani...juzi tuliambiwa kuwa ataanza mazoezi kesho (jana) lakini jamaa leo (jana) hatumuoni," alisikika shabiki mmoja aliyekuwa na bendera ya Yanga mkononi.

"Kama kuna tatizo lolote viongozi wetu watutaarifu na ikiwezekana watuambie ni siku gani atajiunga na wezake kwa ajili ya mazoezi," alisema shabiki mwingine aliyejitambulisha Ramadhan Said huku akiungwa mkono na mashabiki wenzake waliokuwa wakindelea kufuatilia mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kaunda.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa timu hiyo, Fred Minziro 'Majeshi' alisema kuwa mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na wenzake leo tayari kwa maandalizi ya michuano ya Kagame na ile ya Ligi Kuu.

Mchezaji mpya aliyejiunga na klabu hiyo jana ni aliyekuwa beki wa Toto African ya jijini Mwanza, Ladslaus Mbogo ambaye pia amepokelewa kwa shangwe na mashabiki wa timu hiyo na kuwaahidi kuwa atawatumika kwa nguvu zake zote.

Nyota wapya waliojiunga na Yanga msimu huu ambao hadi sasa wameshawasili klabuni hapo ni Nizar Khalfan, Juma Abdur, Said Bahanuzi, Ally Mustafa 'Barthez', pamoja na Mbogo.

Kwa upande wa Simba, nyota wapya; 'Mkongoman' Nkanu Mbiyavanga, Abdalah Juma pamoja na Salum Kinje walionekana kuwa kivutio kwa mashabiki waliojitokeza katika mazoezi hayo kwenye Viwanja vya klabu ya Sigara, TCC Chang'ombe baada ya kuonyesha ufundi na kunogesha mazoezi hayo.

Mazoezi hayo yaliyokuwa yanaendeshwa na Kocha Msaidizi, Richard Amatre yalikuwa ya aina yake huku akitumia muda mwingi katika mazoezi ya kufumania nyavu, kukaba na alikuwa akitumia zaidi.

Mbali na mazoezi hayo pia kocha huyo aliwatumia zaidi wachezaji ambao wapo kikosi cha Simba B kutokana na wachezaji wengine wa timu hiyo waliokuwa timu ya taifa kushindwa kuripoti kwa wakati.

Wakiwa wanafundishwa jinsi ya kuwatoka mabeki na kufunga kwa ustadi, wachezaji waliokua kivutio zaidi ni Salum Kinje aliyekuwa akipiga pasi maridadi sambamba na mwenzake Mbyavanga  pamoja na Abdala Juma aliyesajiliwa kutoka JKT Ruvu ambae alikua akitumia urefu wake kuwachanganya mabeki.

Kocha huyo pia alikua akitumia mazoezi ya kukimbia kwa kasi kwa madai anataka wachezaji hao kuongeza stamina zaidi kwani ndilo tatizo linalowakuta wachezaji wengi.

Baada ya mazoezi hayo, Amatre alisema ameridhishwa na uwezo wa wachezaji wake huku akidai wamekuwa wakifanya vizuri na kusema anamini watafanya vyema katika michuano ya Kagame itakayoanza mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment