Jengo la ofisi ya CCM mkoa wa Singida. (Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida kimewaonya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi watakaobainika kuzunguka kuomba kura kwa wajumbe wakati muda wa kufanya hivyo bado haujafika, majina yao yataondolewa kwenye orodha ya wagombea katika uchaguzi ujao.
Onyo hilo limetolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Singida Naomi Kapambala, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya maamuzi yaliyotolewa na halmashauri kuu katika mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Akifafanua, amesema katika siku za karibuni kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama, kwamba kuna baadhi ya wanachama tayari wameanza kupitapita vijijini kuwarubuni wajumbe ili wawachague kwenye uchaguzi ujao.
Kapambala amesema chama mkoa kikipata ushahidi wa kutosha dhidi ya wanachama hao kuanza kampeni mapema, hakitasita kuwafutilia mbali wananchama hao wanaofanya mambo kinyume na taratibu.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo amesema CCM mkoa, imefanikiwa kunyakua nafasi za uenyekiti wa vijiji 14 na vitongoji 35 katika uchaguzi wa serikali za vijiji uliofanyika Mei 20 mwaka huu.
Kapambala amesema kati ya vijiji 16 vilivyokuwa havina uongozi, CCM ilinyakua vijiji 14 na vijiji viwili vimechukuliwa na CHADEMA.
Amesema vitongoji 37 vilivyokuwa wazi, CCM ilishinda kwa kishindo kwa kunyakua 35,huku CHADEMA ikiambulia viwili tu.
No comments:
Post a Comment