Thursday, May 3, 2012

NENO LA LEO NA MAGGID MJENGWA: PRAVDA NA IZVESTIA- UKWELI NA HABARI!

Ndugu zangu,
Leo ni Siku ya Uhuru wa Habari duniani. Ni siku inayotuhusu sote.
Enzi za Ukomunisti kwenye Soviet Union  kulikuwa na magazeti mawili makubwa; Pravda na Izvestia, ikiwa na maana ya Ukweli na Habari.
Na Urusi kulikuwa na utani mitaani; kwamba kwenye Pravda hakukuwa na ukweli wowote ulioandikwa, na kwenye Izvestia hakukuwa na habari!
Na kwa kiasi kikubwa watu wa mitaani  hawakutania. Huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe. Chama cha Kikomunisti kiliendesha zaidi propaganda. Na tafsiri  sahihi ya propaganda ni uongo. Na propaganda maana yake haswa ni uongo unaorudiwa rudiwa sana hadi pale jamii inapoamini kuwa ni ukweli. Kule Soviet Union, kitengo cha propaganda kwenye Chama Cha Kikomunisti kilikuwa na kazi moja kubwa; kusambaza uongo.
Na anayeajiriwa kufanya kazi hapo lazima moja ya sifa zake ziwe ni umahiri wa kusema uongo. Kwamba hata kama kinachoonekana na kila mmoja kuwa ni jiwe,  mtu wa propaganda anaweza kusema hilo si jiwe, ni mchanga uliolundikana na kufanya kichuguu. Na atarudia rudia kusema hilo mpaka pale wengine mtakapoanza kuamini kuwa mnaliliona mbele yenu si jiwe ni ‘ mchanga uliolundikana’!
Na ukweli una sifa moja kubwa, kuwa hata ukifichwa chini ya uvungu wa kitanda kwa miaka hamsini ( Nusu karne) , iko siku, utatoka na kutembea hadharani wenyewe.  Hautasubiri kuvalishwa viatu.
Yes, get up stand up!
You can fool some people sometimes. But you can’t fool all the people all the time- Bob Marley.
( Pichani nikiwa na wapambanaji; John Bwire na Kyaruzi, Sinza Kijiweni, enzi hizo nikiandikia Rai)


No comments:

Post a Comment