Wednesday, May 16, 2012

SERIKALI YA CUBA YADHAMIRIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA ZANZIBAR.

Kikao cha pamoja kati ya Ujumbe wa Zanzibar ulioongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wa Wizara ya Afya ya Cuba Ulioongozwa na Waziri wake Bwana Roberto Morales Ojeda.Kikao hicho kilifanyika Makao Makuu ya Wizara ya Afya ya Cuba Mjini Havana Nchini Cuba .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi zawadi Waziri wa Afya wa Cuba Bwana Roberto Morales Ojedo ikiwa ishara ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Zanzibar na Cuba. Nyuma ya Bwana Roberto ni Mkalimali wake Bibi Yeny Echevarria.
Mkuu wa watembezaji Wageni katika msitu wa La Moka nje kidogo ya Mji wa Havana Nchini Cuba Bwana Oriol Blaneo Chirino akifafanua Historia ya Msitu huo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ziara yake alipotembelea Msitu huo akiuongoza Ujumbe wa Zanzibar. Kutoka kushoto ni Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji, Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleman Iddi, Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dr. Malik Abdulla Juma, na Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d.
Mkuu wa watembezaji Wageni katika Msitu wa La Moka Bwana Oriol Balaneo Chirino akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuhusu historia ya Kinu cha Kusagia Kahawa katika moja ya eneo la Kihistoria liliomo ndani ya Msitu. Miti kadhaa ya buni kutoka Ufaransa ilioteshwa kwenye msitu huo tokea mwaka 1802.
Serikali ya Jamuhuri ya Cuba inakusudia kuongeza nguvu zake katika Huduma za Afya sambamba na kuendelea kutoa Taaluma kwa Madaktari Wazalendo ili kuona Zanzibar inafikia lengo lake la kuwa na huduma bora za Afya kwa Wananchi wake. 
 Waziri wa Afya wa Nchi hiyo Bwana Roberto Morales Ojeda alieleza hayo hapo Ofisini kwake Mjini Havana Cuba wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ukiwa mwishoni mwa ziara yake ya Kiserikali Nchini Cuba. 
 Bwana Roberto alisema licha ya changamoto ya Uchumi inayoikabili Dunia hivi sasa na hasa katika Mataifa machanga lakini Sekta ya Afya itaendelea kupewa msukumo zaidi kwa Mataifa hayo mawili. Hata hivyo Bwana Roberto alifahamisha kwamba bila ya Maendeleo ya uhakika ya Uchumi Sekta hiyo muhimu katika ustawi wa Jamii inaweza kuyumba na matokeo yake kuleta usumbufu kwa Wananchi walio wengi. 
 Waziri wa Afya wa Cuba alimueleza Balozi Seif kwamba Cuba imeweza kupiga hatua kubwa katika masuala ya Afya hali iliyopelekea kuwa na urafiki wa takriban Mataifa 68 Duniani. Bwana Roberto alieleza kwamba huduma za afya zimepanuka na kufikia asilimia 4.5% mwaka 2011 kwa kufanikiwa kuzuia maradhi zaidi ya 30 sambamba na kufaulu kwa Madaktari 47,000 waliomaliza mafunzo yao katika ngazi yaVyuo Kikuu. “ Sekta ya Afya kwa kweli ndio inayounganisha Watu wa Nchi na Makabila Tofauti Duniani katika Ushirikiano wa Kijamii”. 
Alisisitiza Bwana Roberto. Aliipongeza Zanzibar katika harakati zake za kuwa na Mpango maalum wa kuimarisha Vituo vya Afya kwenye masafa ya Kilomita Tano hatua ambao inakwenda sambamba na Mpango wa Kimataifa wa Milenia . 
 Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa Pamoja na Waziri wa Afya wa Zanzibar Mh. Juma Duni Haji pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Malik Abdulla Juma katika Ujumbe huo ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Cuba kwa mchango wake kwa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika Masuala ya Afya. 
 Balozi Seif alieleza kuwa yapo matumaini mazuri kwa Zanzibar kujisogeza zaidi katika huduma bora za Afya kutokana na Mpango wake wa kuwapatia Mafunzo Madaktari Wazalendo chini ya Wataalamu kutoka Cuba ambao wanatarajiwa kutoa Huduma katika Vituo mbali mbali vya Afya Unguja na Pemba. 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba Jamuhuri ya Cuba imekuwa Mshirika mkubwa wa Tanzania na pia Zanzibar tokea pande hizo mbili zilipojipatia uhuru wao kwa zaidi ya miaka arubaini iliyopita. Mapema Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji aliueleza Ujumbe huo wa Wizara ya Afya wa Cuba Kwamba Wizara yake inakusudia kuufanya Mpango wake wa Mafunzo kwa Madaktari wake kuwa wa kudumu. 
 Waziri Duni alisema jumla ya wanafunzi 153 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo chini ya usimamizi wa chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } ‘ Wizara ya Afya Zanzibar tayari imeshawapatia mafunzo wanafunzi 38 wakiwa mwaka wa tatu wakati Wanafunzi 11 wanaendelea kwa mwaka wa pili chini ya Walimu kutoka Cuba.


No comments:

Post a Comment