Monday, May 28, 2012

WANAFUNZI MKOANI SINGIDA WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF).


Afisa madai wa mfuko wa bima ya afya kanda ya kati Mary Kalogeris akitoa mada yake ya mfuko wa afya ya jamii kwenye semina iliyohudhuriwa na wanafunzi wa walimu wa shule ya sekondari Itigi wilayani Manyoni.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Itigi wilayani Manyoni wakifuatilia kwa makini mada ya mfuko wa afya ya jamii iliyokuwa ikitolewa na afisa madai wa mfuko wa bima ya afya kanda ya kati Bi. Mary Kalogeris (hayupo kwenye picha). (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Afisa madai wa mfuko wa bima ya afya kanda ya kati Mary Kalogeris amewahimiza wanafunzi mkoani Singida, kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) ili pindi wanapougua, asiwasumbue wazazi au walezi wao.
Bi. Mary ametoa wito huo wakati akitoa mada yake  ya faida za kujiunga na CHF, kwenye semina ya siku moja iiyohuduriwa na wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari ya Itigi wilayani Manyoni.
Akifafanua amesema ili mwanafunzi aweze kuwa mwanachama wa mfuko huo, anapaswa kujiunga na wanafunzi wenzake wanne ambao kwa ujumla wao, watakuwa watano huku kila mmoja atalipia  uanachama shilingi elfu moja tu.
Mary amesema wanafunzi wakifanya uamuzi huo wa busara wa kujiunga na CHF, sio tu watakuwa wamejihakikishia kupata tiba ya uhakika, pia watakuwa wamewapunguzia wazazi/walezi usumbufu kutafuta  gharama za matibabu.
Amesema kwa hali hiyo, upo umhimu mkubwa kwa wanafunzi na wananchi wengine kwa ujumla kujiunga na mfuko wa CHF, ambao mwanachama wake anatibiwa bila kutozwa cho chote cha ziada.
Aidha Afisa huyo amewataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri katika kuwahimiza wazazi/walezi wao, nao pia waweze kujiunga na mfuko wa afya ya jamii.
Kwa mujibu wa Bi. Mary, ili kaya yenye mume, mke na watoto wanne walio na umri wa chin ya miaka 18, waweze kuwa wanachama wa CHF, wanapaswa kulipa ada ya kiingilio shilingi 5,000 tu ma wanapolipa ada hiyo, watatibiwa bila gharama yo yote kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kati ya kaya 52,513 za wilaya ya manyoni, ni kaya 1,317 sawa na asilimia tano tu, ndizo zilizojiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF).


No comments:

Post a Comment