Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wana soka wa Mkoa wa Kaskazini Unguja chini ya umri wa miaka 17 katika hafla ya kuifunga rasmi kambi yao katika Jengo la kituo cha Huduma rafiki Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja. Timu hiyo inatarajia kuwa miongoni mwa wana michezo watakaoshiriki kwenye mashindano ya Copa Coca Cola yatakayoanza Jijini Dar es salaam Mwishoni mwa Wiki hii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifunga rasmi Kambi ya Timu ya Soka ya Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Jengo la Kituo cha Huduma Rafiki Mahonda. Kulia Ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na Ameir Katibu wa CCM Wilaya na Kaskazini B. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Kaskazini “A” Khamis Kombo.
Makamu wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi mchango wa Shilingi 700,000/- kwa Mkuu wa Msafara wa Timu ya Mkoa Kaskazini Unguja ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Kaskazini B Omar Ali Khamis. Mchango huo ni kwa ajili ya ununuzi wa Viatu kwa Timu ya Soka ya Vijana wa Mkoa huo watakaoshiriki Mashindano ya Copa Coca Cola Jijini Dar es salaam yanayotarajiwa kuanza Mwishoni mwa Wiki hii. (Picha na Saleh Masoud Mahmoud OMPR-ZNZ).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni mbunge wa Jimbo la kitope Balozi Seif Ali Iddi amevutiwa na moyo na kauli ya wanamichezo wa Timu ya Soka ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ya kwenda kushinda katika mashindano ya Copa Coca Cola yanayoanza Mwishoni mwa Wiki hii Mjini Dar es salaam.
Balozi Seif ametoa Kauli hiyo mapema wakati alipoitembelea Kambi ya Vijana 20 na Viongozi 7 wa Timu hiyo na kuifunga rasmi katika jengo la Kituo cha Huduma Rafiki Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema yeye pamoja na Viongozi wenzake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watajitahidi kuhakikisha ushiriki wao kwenye mashindano hayo hautakuwa na Matatizo.
Amewakumbusha kwamba cha kuzingatia zaidi ni Ushirikiano baina yao na wenzao kwenye mashindano hayo kwa vile Michezo mbali ya Mashindano lakini mara nyingi hujenga na kuleta Urafiki.
Balozi Seif katika kujenga Mazingira mazuri ya ushindi kwa Wanamichezo hao amekabidhi Mchango wa Shilingi Laki Saba Taslim (700,000) kwa ajili ya ununuzi wa Viatu ili wafikie daraja la kucheza katika mfumo wa Kisasa wa Mchezo huo.
Amewaomba safari yao ya Mashindano iwe ya kushinda na sio kushiriki kwa vile mara zote kwenye michezo ipo sifa ya kushinda na si vyenginevyo.
Balozi Seif amesema hitilafu ndogo ndogo katika michezo haiwezi kuepukika lakini kinachowapasa Vijana hao kuzingatia zaidi ni nidhamu na kuepuka hasira wakati wawapo Viwanjani.
Ameahidi kuwatembelea watakapokuwa Mashindanoni iwapo wakati utamruhusu endapo atapata wasaa wa kupita Mjini Dar es salaam katika majukumu yake ya kikazi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Viongozi wa Serikali na ZFA wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa juhudi zao za kukaa nao pamoja Wanamichezo hao kwenye Kambi hiyo.
Amesema Kitendo hicho cha kuwanoa Vijana hao kinaashiria mategemeo makubwa ya Wawakilishi hao wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kufanya vizuri katika mashindano hao.
Katika Risala yao iliyosomwa na Mshika Fedha wa ZFA Wilaya ya Kaskazini “B” Mosi Ame Mosi Wanamichezo hao wamempongeza Balozi Seif kwa moyo wake wa kijasiri uliopelekea kuwajengea hamasa ya kurejea Mkoani humo na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Mosi Ame Mosi amemueleza Balozi Seif kwamba Vijana hao wa umri wa chini ya Miaka 17 wamewiva na wako tayari kimashindano licha ya matatizo madogo madogo ambayo si kikwazo katika malengo yao ya ushindi.
Mashindano ya Copa Coca Cola yaliyoandaliwa na Kampuni ya Coca Cola Tanzania yanatarajiwa kuanza Tarehe 23 June 2012 katika Viwanja vya Karume, Kawe pamoja na Tamco na kumalizika Tarehe 6 Julai 2012 yakijumuisha takriban Makundi manne.
No comments:
Post a Comment